Jumuiya ya Madola yaihimiza Uganda kumuwachia Besigye
18 Februari 2025Jumuiya ya Madola imeitolea wito Uganda, ambayo ni mwanachama wa kundi hilo la mataifa 56, kumuwachia huru mwanasiasa wa upinzani Kizza Besigye.
Jumuiya hiyo imesema kuzuiliwa kwake kunahujumu demokrasia na haki za binaadamu. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Patricia Scotland amesema jumuiya hiyo siku zote imekuwa na uhusiano unaotegemea kuaminiana na Uganda na inatarajia kurejea kwa mazingira jumuishi zaidi ya kisiasa na ya kidemokrasia yanayoambatana na Mkataba wa Jumuiya ya Madola".
Besigye, mkosoaji wa muda mrefu wa Rais Yoweri Museveni, alishtakiwa kwenye mahakama ya kijeshi na amekuwa gerezani kwa karibu miezi mitatu kwa mashitaka yakiwemo kumiliki silaha kinyume cha sheria. Hatua hiyo imezusha hasira na ukosoaji dhidi ya serikali. Besigye mwenye umri wa miaka 68, alianza mgomo wa kula wiki iliyopita, na akapelekwa hospitali kwa muda mfupi mwishoni mwa wiki. Hii leo yamefanyika maandamano mjini Kampala ya kutaka mwanasiasa huyo aachiwe huru.