Jumuiya ya kimataifa yaunga mkono mpito mpya wa Syria
15 Februari 2025Takriban nchi 20, zikiwemo Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Canada, na Japan, zimeahidi kushirikiana kuhakikisha mpito wa Syria baada ya kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad unafanikiwa. Mkutano wa Paris umeahidi kusaidia mamlaka mpya za Syria katika mapambano dhidi ya ugaidi na msimamo mkali.
Serikali mpya ya mpito inajaribu kushawishi mataifa ya Magharibi kulegeza vikwazo vilivyowekwa dhidi ya utawala wa Assad ili kusaidia katika ujenzi wa uchumi wa nchi hiyo baada ya vita vya miaka 14. Umoja wa Ulaya na Marekani tayari zimeanza kulegeza baadhi ya vikwazo, hasa katika sekta ya nishati.
Soma pia: Erdogan amsifu rais mpya wa Syria kwa kudhamiria kupambana na ugaidi
Kuna mashaka miongoni mwa mataifa ya Magharibi kuhusu mwelekeo wa uongozi mpya wa Syria, hususan katika uhuru wa kidini, haki za wanawake, na haki za jamii ya Wakurdi. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock, amesisitiza kuwa ni muhimu kwa makundi yote kushirikishwa katika uongozi wa nchi hiyo.