Jumuiya ya Kiarabu yasisitiza Amani Mashariki ya Kati
6 Septemba 2025Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imesema haitowezekana kuishi pamoja kwa amani katika eneo la Mashariki ya Kati bila kuwepo taifa huru la Palestina na kukomesha kile walichokitaja kuwa vitendo vya Israel vya kuendeleza uhasama.
Katika azimio lililowasilishwa na Misri na Saudi Arabia, Jumuiya hiyo imesema kushindwa kufikia suluhisho la haki katika kadhia ya Palestina na uhasama wa utawala unaoikalia kwa mabavu bado ni vikwazo vikubwa vinavyozuia jitihada za kuishi pamoja kwa amani katika eneo hilo.
Azimio hilo ni sehemu ya mkutano mpana uliofanyika mjini Cairo, Misri ambapo mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Kiarabu waliidhinisha Dira ya Pamoja ya Usalama na Ushirikiano katika Kanda ya Mashariki ya Kati.
Mkutano huo umefanyika wakati jeshi la Israel likizidisha mashambulizi yake katika mji wa Gaza City. Wakati huo huo Msemaji wa jeshi la Israel Avichay Adraee, amewataka wakaazi wa Gaza City, kuondoka na kwenda kwenye eneo salama la kusini kabla ya kuanza operesheni ya kijeshi ya kulidhibiti kikamilifu eneo la kati la Gaza City. Jeshi la Israel limesema watu wanatakiwa kwenda katika eneo la Al-Mawasi huko Khan Younis.