Juhudi za kuvimaliza vita vya Ukraine zaendelea
11 Julai 2025Wakati juhudi za kidiplomasia, misaada ya kimataifa, na msukumo wa vikwazo dhidi ya Urusi vikiendelea kuongezeka, mataifa mbalimbali yanaonesha dhamira ya kuisaidia Ukraine kijeshi na kiuchumi, huku hali ya usalama, misaada ya kibinadamu na nafasi ya suluhu ya amani vikiwa bado ni masuala yenye mvutano mkubwa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov na mwenzake wa Marekani Marco Rubio walikutana kwa mazungumzo katika mji mkuu wa Malaysia wa Kuala Lumpur kando ya mkutano wa ASEAN na kujadili kuhusu vita vya Ukraine lakini kulikuwa na matarajio hafifu ya kufikia mafanikio yoyote.
Viongozi hao walikutana saa chache baada ya Moscow kuushambulia vikali mji mkuu wa Ukraine Kyiv kwa usiku wa pili mfululizo huku Umoja wa Mataifa ukitahadharisha kuwa idadi ya wahanga wa mashambulizi ya Urusi imefikia kiwango cha juu zaidi.
Zelensky atoa wito wa kupewa silaha zaidi
Kufuatia wito wa rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky wa kuitaka Marekani kuipatia silaha zaidi, Katibu mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Mark Rutte amesema amezungumza na Trump na wanashirikiana kwa karibu na washirika wengine wa Magharibi ili kuipatia Ukraine msaada inaouhitaji.
Wakati Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni akihimiza vikwazo zaidi dhidi ya Urusi, Ujerumani imesema inajiandaa kununua mifumo ya ulinzi wa makombora ya Patriot kwa ajili ya Ukraine. Aidha, viongozi wa Uingereza na Ufaransa wakitangaza kuandaa mipango ya kutumwa kwa kikosi cha kulinda amani nchini Ukraine ikiwa kutafikiwa makubaliano ya usitishaji mapigano.
Jana mjini Rome, viongozi wa Ulaya walizindua mkutano wa kila mwaka wa kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Ukraine baada ya vita wakitarajia kukusanya dola bilioni 12, huku wakiwatolewa wito wamiliki wa makampuni na watu binafsi kuwekeza katika miradi itakayosaidia mpango huo.
Yote hayo yakiarifira, watu wawili wameripotiwa kuuawa na wengine 26 wamejeruhiwa nchini Ukraine kufuatia wimbi jipya la mashambulizi ya Urusi mjini Kyiv. Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema kuwa imedungua droni nne za Ukraine zilizokuwa zimeelekezwa Moscow na hivo kutatiza kwa muda shughuli katika viwanja vitatu vya ndege.