Juhudi za kupambana na Mpox zaimarishwa Kenya
31 Julai 2025Wizara ya afya nchini Kenya imeimarisha ushirikiano na serikali za majimbo hasa yaliyoripoti maambukizi ya ugonjwa wa Mpox baada ya ugonjwa huu kuendelea kusambaa, katika majimbo ya Mombasa, pwani ya Kenya ambako kuna visa 139 vilivyothibitishwa na Busia, magharibi ya Kenya visa 69.
Mkurugenzi Mkuu wa Afya katika wizara ya afya ya Kenya Dokta Patrick Amoth anasema wameweka mipango ya kupunguza maambukizi zaidi na udhibiti sawia na kuweka mifumo ya utambuzi wa haraka na ufuatiliaji wa waliotangamana na walioambukizwa ugonjwa huo huku juhudi zaidi sasa zikielekezwa Mombasa baada ya jimbo hilo kuathirika zaidi.
"Mombasa sasa ndio kitovu cha ugonjwa huu, tutaendelea kushirikiana na serikali zetu za majimbo kuimarisha juuhudi za udhibiti, sawia na kuimarisha ushirikiano wa kijamii na kuhakikisha visa vyote vinadhibitiwa."
Baadhi ya maambukizi yamehusishwa na watu kusafiri kutoka mataifa jirani kama vile Uganda na Rwanda huku uchuguzi wa vipimo ukiimarishwa mipakani na maeneo ya bandari.
Zaidi ya wasafiri 930,000 wachunguzwa katika vituo 26 vya kuingia nchini
Katika eneo la magharibi ya Kenya, kando na Busia inayopakana na taifa la Uganda, majimbo mengine yaliyoathirika ni Bungoma iliyosajili visa vitatu vya maambukizi, jimbo la Kakamega likiwa la hivi karibuni kuandikisha maambukizi mapya ya visa vitatu vya wagonjwa waliothibitishwa kuugua ugonjwa huo.
Fernandes Barasa gavana wa Kakamega anaeleza kuwa wagonjwa watatu waliothibitishwa kuambukizwa jimboni humo wametengwa kwa kipindi cha siku 21 hadi hali yao ya kiafya itakapokuwa imara.
"Tunashugulika na kuhakikisha wamepata matibabu na kuhakikisha hawaendi popote kwa siku 21, kwa sababu ugonjwa huu unaambukiza, na pia watu sita wa familia zao tumewaweka katika karantini."
Mpox huenea kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kwa kuwa karibu na mgonjwa aliyeambukizwa kupitia kugusana ngozi, kupumua hewa na pia inasambaa kupitia ngono, sawia na uwezekano wa kusambaa kupitia kugusa vitu vilivyoguswa au kutumika na mwathiriwa wa virusi mfano, nguo, kitambaa cha kufuta jasho, kamasi na pia vifaa vya kulalia kama vile mashuka, mito na godoro.
Afisa wa afya ya umma Sylgade Wasike amesema, "Ili kuzuia, tunahimiza umma kuripoti katika vituo vya afya vilivyoko karibu kwa walioonyesha ishara na dalili na tunawahimiza kuimarisha usafi, hasa usafi wa mikono, ili waoshe kwa sabuni na maji."
Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na kutoka vipele usoni, mikononi, miguuni na sehemu zingine mwilini, uvimbe mwilini, maumivu makali ya kichwa, mgongo na misuli. Upele huwa na mwasho sana.
Kaunti ya Nairobi imeripoti visa 13, Nakuru 23 miongoni mwa majimbo mengine.