Juhudi za kumaliza mzozo wa Kongo na Rwanda zaimarika
4 Septemba 2025Kikao hicho kiliwahusisha wapatanishi kutoka Qatar, Marekani, Togo na Kamisheni ya Umoja wa Afrika, kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Jumatano.
Taarifa hiyo ilikiri kuwa utekelezaji wa baadhi ya vipengele vya makubaliano ya awali umekuwa wa kusuasua. Hata hivyo, Rwanda na DRC zilikubaliana kuanzisha njia ya kiufundi ya kubadilishana taarifa za kiusalama na kijeshi kabla ya kikao kijacho cha kamati hiyo kitakachofanyika Doha, Qatar. Togo iliwakilisha Umoja wa Afrika katika kikao hicho.
Wakati huo huo, serikali ya DRC imetangaza kuwa kampuni ya uwekezaji ya Qatar, Al Mansour Holdings, inalenga kuwekeza dola bilioni 21 nchini humo, huku Doha ikiendelea kusimamia juhudi za kuleta amani mashariki mwa nchi.
Mwanzilishi wa kampuni hiyo na pia mwanafamilia wa kifalme, Sheikh Mansour bin Jabor bin Jassim Al Thani, alitembelea mji mkuu Kinshasa Jumanne kama sehemu ya ziara yake barani Afrika.
Qatar iliwasilisha nia ya kuwekeza Kongo mwezi Agosti
Katika kikao chake na Waziri Mkuu Judith Suminwa ujumbe wa Qatar uliwasilisha barua ya nia ya kuwekeza kwenye sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, fedha, madini, dawa na gesi asilia. Hata hivyo, afisa mmoja wa Qatar aliliambia shirika la habari la AFP kwamba ziara ya Sheikh Mansour ilikuwa ya kibinafsi ya kibiashara.
Mwezi uliopita, Al Mansour Holdings pia iliahidi uwekezaji wa dola bilioni 70 katika nchi nne za Kusini mwa Afrika — Botswana, Msumbiji, Zambia na Zimbabwe — wakati nchi hizo maskini zenye rasilimali nyingi zikikabiliwa na kupunguzwa kwa misaada ya Marekani tangu kurejea madarakani kwa Rais Donald Trump.
Mapigano katika eneo lenye utajiri wa madini mashariki mwa DRC yaliongezeka mapema mwaka huu baada ya kundi la waasi la M23 linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda kuanzisha mashambulizi makali na kuteka miji mikuu miwili ya majimbo ndani ya muda wa wiki chache.
Juhudi za kidiplomasia zilikuwa zimeshindikana hadi katikati ya Machi pale Qatar ilipotangaza kwa ghafla kuwa Rais wa Rwanda Paul Kagame na Rais wa DRC Felix Tshisekedi walikutana mjini Doha kwa mazungumzo.
Mnamo Juni, mataifa hayo mawili yalitia saini makubaliano ya amani mjini Washington. Sambamba na hilo, serikali ya Kongo na waasi wa M23 walifanya mazungumzo mjini Doha mwezi Aprili na kuafikiana mwezi Julai juu ya kusitisha mapigano. Hata hivyo, mapigano bado yanaendelea mashinani.