Joto kali limeathiri vinu vya umeme
31 Julai 2006Kwa sababu ya joto hilo kali lililoanza kati kati ya mwezi wa Juni,serikali nchini Ufaransa, Ujerumani,Hispania na kwengine barani Ulaya, zimelazimika kwenda kinyume na sheria zake zenyewe kuhusika na mazingira.Kuambatana na sheria hizo,vinu vya nishati huruhusiwa kumwaga mitoni,maji yanayopooza vinu hivyo,yakiwa na joto fulani. Lakini Julai 24,serikali ya Ufaransa ilitangaza kuwa vinu vya nishati ya kinuklia vilivyo kando ya mito,vitaruhusiwa kumwaga maji ya moto katika mito hiyo.Hatua hiyo imechukuliwa kuhakikisha kuwa nchi itaendelea kupata umeme.Ufaransa ina jumla ya vinu 58 vya kinuklia ambavyo huzalisha takriban asili mia 80 ya nishati inayotumiwa nchini humo.Vinu 37 vipo karibu na mito ambayo hutumiwa na vinu hivyo,kumimina maji yanayopooza mitambo yake.Kuna hatari kuwa baadhi ya mitambo itapaswa kufungwa kwani ukame uliosababishwa na majira ya joto kali sana,umepunguza maji mitoni.
Katika hali za kawaida,sheria za mazingira zenye azma ya kuhifadhi mimea na viumbe vinavyoishi mitoni,hupiga marufuku kumimina katika mito hiyo,maji yaliyozidi joto fulani.
Kwa hivi sasa Ufaransa inaagizia umeme kutoka nchi za jirani kufidia upungufu uliotokea katika vinu vyake vya kinuklia.
Wakati Ufaransa imefumba macho kuhusu sheria za mazingira,huku nchini Ujerumani,mashirika ya nishati ya kinuklia yamerekebisha vinu vyake kwa azma ya kupunguza joto wa maji machafu na kuhifadhi mimea na viumbe majini.Vinu vyote vya kuzalisha nishati ya kinuklia,karibu na mito,vimechukua hatua hiyo.Hata mitambo ya desturi inayotumia visukuku kutengeneza umeme vimefanya hivyo hivyo.
Hispania,nako kwenye vinu 8 vinavyotoa nishati ya kinuklia,kimoja kimefungwa kwa sababu ya joto kubwa lililopimwa katika mto Ebro ambao hutumiwa na kinu hicho kuyamwaga maji yanayopooza mitambo yake.Kinu hicho kilicho Santa Maria de Garona ni cha zamani kabisa nchini Hispania na hutoa asili mia 20 ya umeme nchini humo.
Kwa mujibu wa mtaalamu wa nishati nchini Ujerumani,Hermann Scheer,hali ya hivi sasa inadhihirisha haja ya kufanywa mageuzi makubwa katika sera za nishati.Amesema,pesa zaidi lazima zitumiwe kwa miradi ya nishati mbadala na vinu vya kinuklia vifungwe upesi iwezekanavyo.
Hata nchini Ufaransa,mtaalamu wa sayansi ya kinuklia,Hubert Reeves ameihimiza serikali itoe pesa zaidi kwa ajili ya nishati mbadala. Amesema,tunapaswa kuachilia mbali nishati ya kinyuklia na tushughulikie nishati mbadala.