Joto kali laihangaisha Ulaya
1 Julai 2025Nchi mbali mbali barani Ulaya zinakabiliwa na hali ya hewa ya joto na jua kali wakati huu, huku idara za afya zikitahadharisha kuhusu madhara ya hali hiyo. Idara ya Utabiri wa hali ya hewa hapa nchini Ujerumani imesema joto kali zaidi litashuhudiwa kesho Jumatano.
Kuanzia nchini Ufaransa, Ubelgiji, Uholanzi, Ujerumani, Uhispania mpaka Uingereza joto na jua kali ndiyo hali ya hewa inayoshuhudiwa kwa sasa, ikielezwa kwamba ndilo joto kali zaidi katika majira ya kiangazi kuwahi kushuhudiwa mwaka huu. Joto limeongezeka hii leo huko Paris nchini Ufaransa, Ubelgiji na Uholanzi huku likielezwa kushuka kiasi nchini Ureno ambako hakujatolewa tahadhari ya hatari ya joto hilo kali.
Christel ni mtalii kutoka Canada anayetembelea Paris amesema joto limezidi. "Kwahakika joto ni kali sana tunakunywa maji mengi sana na nafikiri mji wenyewe ni mzuri na tunabahati kuitembelea Ufaransa na Paris''
Charlie Ghorst naye anatokea Marekani anaitembelea London anasema huko pia joto sio la kawaida."Joto ni kali mno. Kwa kusema kweli ni changamoto kiasi kwa sababu hakuna upepo hata kidogo ni kana kwamba unazowea hali ya hewa ya joto kali lakini ambayo haina hata kiupepo kidogo na kwa hakika ni ngumu.''
Hali ya tahadhari nchini Ufaransa
Nchini Ufaransa, idara ya hali ya hewa Meteo-France imeziweka idara nyingi za nchini humo katika tahadhari kubwa huku mji wa Paris hasa ukiwa katika hali mbaya zaidi ya joto kali. Joto linategemewa kuongezeka Jumanne huku shule zaidi ya 1300 zikitarajiwa kufungwa kabisa au kuendelea kwa muda mfupi. Nchini Ujerumani nako hali pia ni mbaya,Tim Staeger kutoka Kituo cha hali ya hewa mjini Frankfurt amesema joto kali zaidi litashuhudiwa Jumatano. ''Joto kali litafikia kilele chake Jumatano ambapo kiwango cha joto kitafikia zaidi ya nyuzi 35 katika maeneo ya magharibi mwa nchi katika eneo la mto Rhine na katika eneo la Ruhr itafikia mpaka zaidi ya nyuzi 39. Hata hivyo bado hilo sio joto la kuvunja rekodi Ujerumani nzima. Katika mji wa Duisburg joto liliwahi kufika hadi nyuzi 41.2 Julai 29 mwaka 2019''
Watalaamu wa maswala ya hali ya hewa wanaonya kwamba hali ya joto kali huenda ikashuhudiwa mara kwa mara katika miaka ijayo wakati wa msimu wa kiangazi na huenda likawa kali zaidi kuliko ilivyowahi kushuhudiwa. Hivi sasa nchini Ufaransa idara ya hali ya hewa imesema pia kwamba joto linatarajiwa kupindukia nyuzi 40 katika kipimo cha Celsius kila mwaka.
Kusitishwa kwa shughuli za utalii
Shughuli za utalii zimesitishwa katika eneo maarufu la mnara wa Eifel hivi leo huku magari pia usafiri wa magari ukipigwa marufuku na kuweka sheria kali za kuzuia uendeshaji magari kwa mwedo wa kasi kubwa.
Nchi za eneo la bahari ya Mediterranea kutoka rasi ya Iberia hadi Ufaransa na Italia hadi eneo la Balkan na Ugiriki kwa siku chungunzima sasa zimekuwa zikihangaishwa na joto na jua kali kiasi cha kuchochea kutolewa tahadhari za kiafya huku kwa upande mwingine tahadhari zikitolewa pia kuhusu kitisho cha kuzuka moto wa nyika.
Japan pia imesema mwezi Juni ulikuwa na joto kali zaidi kuliko kipindi kingine mwaka huu. Wanasayansi wanasema mabadiliko ya tabia nchi yaliyochochewa na binadamu ndiyo chanzo cha matukio haya kuongezeka na kuna hatari ya kuendelea kushuhudiwa na kusambaa.