ICC yawasilisha ushahidi dhidi ya Joseph Kony
8 Septemba 2025Kony anaandamwa na mashtaka kadhaa ya uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita, yakiwemo mauaji, ubakaji na utumwa wa kingono. Anadaiwa kuongoza harakati za kikatili za LRA ziliyoitisha kaskazini mwa Uganda kwa miongo kadhaa.
Kulingana na wachambuzi hatua ya kusikiliza kesi bila kumkamata Kony ni kama jaribio la kuona ikiwa kesi za aina hii zinaweza kutumika dhidi ya watuhumiwa wengine walioko nje ya mamlaka ya ICC mfano Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu au Rais wa Urusi, Vladimir Putin.
Mahakama inasikiliza kesi hiyo si kwa lengo la kutoa hukumu moja kwa moja, bali ni fursa kwa waendesha mashtaka kuwasilisha ushahidi wao. Kony anawakilishwa na wakili wa utetezi, lakini kwa mujibu wa sheria hawezi kuhukumiwa bila kuwepo mahakamani.
Uganda yenyewe itafuatilia kwa karibu
Waathirika na manusura wengi wanasema hata kama Kony hajakamatwa, hatua hii inaleta matumaini ya haki baada ya mateso makubwa
Stella Angel Lanam, ni Mkurugenzi wa Shirika la War Victims and Children Networking Initiative mjini Gulu ambaye amesema "Ukiangalia mambo ambayo watu wa kaskazini mwa Uganda wamepitia kwa miaka hii yote, najua hata Kony hawezi kufidia yote, hata serikali ya nchi pia haiwezi. Nilikuwa na umri wa miaka 10 tu, na niliteseka kwa miaka tisa; je, serikali au Kony watanirudisha jinsi nilivyokuwa? Hapana! Lakini angalau nitapata haki.”
Joseph Kony alikulia katika familia ya Kikatoliki kaskazini mwa Uganda na baadaye akajitangaza kuwa kiongozi wa kidini aliyeitwa na roho mtakatifu kupigana na serikali ya Rais Yoweri Museveni. Mnamo 1987, aliondoka kijijini kwake akiwa na wafuasi 11 pekee kuanzisha vuguvugu lake na kuahidi kuiongoza Uganda kwa kufuata Amri Kumi za Biblia.
Harakati zake ziligeuka kuwa hofu
LRA ilihusishwa na mashambulizi ya kuvizia vijijini, utekaji wa watoto, na ukatili wa kukata viungo. Serikali ya Uganda iliwalazimisha mamia kwa maelfu ya watu kuishi kwenye kambi za wakimbizi wa ndani, hatua iliyoongeza mateso ya raia bila kuondoa tishio la waasi.
Marekani ilijaribu kumtafuta Kony mwaka 2011 kwa kutuma wanajeshi kusaidia jeshi la Umoja wa Afrika na baadaye kutoa zawadi ya hadi dola milioni tano kwa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwake.
Hata hivyo, Kony bado bado hajulikani alipo na inasemekana kujificha mpakani mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati na Darfur Kusini mwa Sudan.
Kony alipata umaarufu wa kimataifa mwaka 2012 kupitia video ya mtandaoni "Kony 2012” iliyotazamwa zaidi ya mara milioni 100. Ingawa kampeni hiyo ilififia haraka, ilirejesha tena mjadala kuhusu kushirikisha vijana na mitandao ya kijamii kwenye mapambano ya haki za binadamu.