Joseph Kabila: Rais wa zamani matata alierudi DR Kongo
30 Mei 2025Baada ya miaka minne ya ukimya tangu kumkabidhi madaraka Felix Tshisekedi mnamo 2019, Joseph Kabila amerudi katika siasa za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), akirudi akiwa hana ndevu na akizungumzia wazi kile alichokiita "udikteta" mpya unaoikumba nchi hiyo.
Kurejea kwake, akiwa na historia ya uongozi wa miaka 18, kumezua taharuki kubwa miongoni mwa viongozi wa serikali ya sasa, hasa ikizingatiwa kuwa ametuhumiwa kuwa na uhusiano wa karibu na waasi wa M23 wanaodaiwa kusaidiwa na Rwanda.
Kabila, mwenye miaka 53, amekuwa mtu wa kujitenga na mwenye kupendelea ukimya. Kwa muda mrefu aliweka hadhi ya kisiasa kimyakimya, hata baada ya kuondoka madarakani kwa mara ya kwanza kwa njia ya amani tangu uhuru wa nchi hiyo kutoka kwa Wabelgiji. Hata hivyo, nyuma ya pazia, ushawishi wake uliendelea kujidhihirisha – na sasa umetangazwa rasmi kuwa tishio.
Serikali imefuta usajili wa chama chake cha People's Party for Reconstruction and Democracy (PPRD), na kuashiria uwezekano wa kumfungulia mashtaka ya uhaini kutokana na tuhuma za kusaidia waasi wa M23 waliouteka mji wa Goma mapema mwaka huu.
Licha ya historia ya utawala wake kuandamwa na tuhuma za ufisadi na usimamizi mbovu, Kabila bado ana mashabiki wanaomuona kama mkombozi aliyesaidia kuleta utulivu baada ya Vita vya Pili vya Kongo – vita ambavyo viligharimu maisha ya zaidi ya watu milioni tatu.
Kiongozi kutoka kanda ya mashariki, anaetiliwa mashaka Kinshasa
Alizaliwa Juni 4, 1971, mashariki mwa DRC – eneo ambalo mara nyingi huonekana kama tofauti na mji mkuu wa Kinshasa, kijiografia na kitamaduni. Alikulia Tanzania baada ya familia yake kukimbia vita, na kurudi DRC mwaka 1996 wakati wa Vita vya Kwanza vya Kongo.
Kabila huongea zaidi Kiswahili na Kiingereza, hali ambayo ilimfanya asieleweke vyema Kinshasa, ambapo wengi huzungumza Lingala. Kutokana na historia yake, baadhi ya Wakongo humuona kama "mgeni” au hata "Mnyarwanda” aliyejinufaisha binafsi na utajiri wa madini wa taifa hilo huku wananchi wake wakiendelea kuteseka.
Wakosoaji wake wanadai aliruhusu mikataba ya madini yenye masharti mabaya, ikiwemo kwa wawekezaji wa kigeni, huku mamilioni ya raia wakipambana kupata huduma za msingi. Hata hivyo, Kabila hujieleza kama kiongozi aliyejitolea kwa unyenyekevu kulitengeneza taifa lililovunjika na kujeruhiwa na historia ya machafuko.
Safari ya kiiasa: Kutoka vita, kuelekea kivuli cha urithi
Kabila aliingia madarakani akiwa na umri wa miaka 29 baada ya kuuawa kwa baba yake, Laurent-Désiré Kabila, mwaka 2001. Alishinda uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia ulioratibiwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2006, lakini ushindi wake wa mwaka 2011 ulizua utata baada ya kiongozi wa upinzani Etienne Tshisekedi – baba yake Felix – kudai wizi wa kura.
Baada ya uchaguzi wa 2018, Kabila alimkabidhi mamlaka Tshisekedi, lakini makubaliano yao ya muungano wa kisiasa yalivunjika ndani ya miaka miwili, na tangu wakati huo Tshisekedi amekuwa akipambana kumweka mbali Kabila kisiasa.
Kurejea kwa Kabila – kwa sauti mpya, bila ndevu na akiwa na ujumbe mkali wa kisiasa – kunaibua maswali kuhusu mustakabali wa siasa za DRC. Je, ni mwanzo wa safari mpya kwa Kabila au hatua ya mwisho ya mtu anayetaka kurudi kwenye kitovu cha mamlaka kwa njia zisizo za moja kwa moja?
Kwa taifa lililobarikiwa na madini lakini linalokumbwa na ukosefu wa usalama, umaskini mkubwa, na mgawanyiko wa kikanda, hatima ya Kabila – na namna serikali itakavyoshughulikia urithi wake – huenda ikatibua au kutatua siasa za DRC kwa miaka mingi ijayo.