Kabila aibukia Goma, azungumza na viongozi wa dini
30 Mei 2025Kabila alikutana siku ya Alhamisi na viongozi wa kidini katika mji wa Goma – miongoni mwa ngome zinazodhibitiwa na waasi wa M23 – akielezea dhamira yake ya kusaidia kurejesha amani katika eneo hilo lenye misukosuko.
Askofu Mkuu Joel Amurani wa Jukwaa la Madhehebu ya Dini alisema Kabila aliwaalika kwa nia ya kuonyesha msimamo wake wa kutaka kuona utulivu ukirejea.
"Tumemweleza kwamba bado ana nafasi ya kubeba jukumu la mpatanishi. Kwa miaka 18 amelitumikia taifa hili, na bado ana uwezo wa kuisaidia nchi kurejea kwenye umoja,” alisema Amurani baada ya kikao hicho.
Kabila, ambaye aliiongoza Kongo kuanzia mwaka 2001 hadi 2019, anakabiliwa na tuhuma nzito za kushiriki katika uasi, uhalifu wa kivita, na uhalifu dhidi ya ubinadamu, hasa kuhusiana na madai ya kuunga mkono waasi wa M23 wanaodaiwa kupata msaada kutoka kwa serikali ya Rwanda. Tuhuma hizo zimeibuliwa na Waziri wa Sheria wa Kongo, Constant Mutamba.
Hatua ya bunge yaibua mjadala kuhusu mustakabali wake kisiasa
Ingawa serikali bado haijatoa taarifa rasmi kuhusu iwapo Kabila atashtakiwa, hatua ya bunge kuidhinisha kuondolewa kwa kinga yake ya "seneta wa maisha" wiki iliyopita, imechochea mijadala mipya kuhusu mustakabali wake wa kisiasa na kisheria.
Wakosoaji wake wanaamini kurejea kwake Goma si wa bahati mbaya bali ni hatua ya kimkakati kujisafisha na kujijenga upya kisiasa katika eneo ambalo linakabiliwa na janga la kibinadamu na ukosefu wa utawala wa sheria.
Kabila alikuwa uhamishoni kwa hiari tangu mwaka 2023, lakini mwezi Aprili alirejea nchini na kuelekea moja kwa moja mashariki mwa Kongo, wakati ambapo serikali ya Rais Félix Tshisekedi inaendelea kukabiliana na changamoto za kiusalama na uaminifu miongoni mwa maafisa wake waandamizi.
Wakati baadhi ya wachambuzi wakitazama kurejea kwake kama juhudi za dhati za upatanishi, wengine wanaona ni mbinu ya kisiasa ya kujinusuru na mikono ya sheria.
Wakati huo huo, waasi wa M23 wameendelea kudhibiti miji mikuu mashariki mwa nchi hiyo licha ya juhudi za kijeshi za serikali. Hali hiyo imewafanya mamilioni ya raia kuyahama makazi yao huku mashirika ya misaada yakionya juu ya janga la kibinadamu linalozidi kushamiri.
Je, kurejea kwa Kabila kutaleta mwelekeo mpya katika mzozo wa mashariki mwa Congo, au ni mwanzo wa sura nyingine ya mvutano wa kisiasa unaofunika uhalisia wa mateso ya wananchi? Muda utatoa majibu.