Jopo laundwa kumaliza mzozo wa Kongo
25 Machi 2025Kwa mujibu wa tangazo rasmi la kuhitimisha mkutano huo wa kilele uliofanyika usiku wa kuamkia leo, jopo la wasuluhishi lililoteuliwa linajumuisha rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo, rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta, rais wa zamani wa Afrika Kusini Kgalema Motlanthe, rais wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Catherine Samba Panza, na rais wa zamani wa Ethiopia Zahle-Work Zewde.Tangazo hilo limeeleza kuwa uteuzi wa jopo hilo umezingatia ukanda, lugha na jinsia.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya SADC, Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe, na yule wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais William Ruto wa Kenya ambao kwa pamoja wameuongoza mkutano huo, wamepewa jukumu la kuwakutanisha wapatanishi hao katika muda wa siku saba, kwa ushirikiano na Umoja wa Afrika.
Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na Rais Paul Kagame wa Rwanda ambaye nchi yake inatuhumiwa kulisaidia kundi la uasi la M23, ni miongoni mwa viongozi waliohudhuria mkutano huo uliofanyika kwa njia ya mtandao.
Jana Jumatatu, rais wa Angola Joao Lourenco alijiondoa katika nafasi ya upatanishi katika mzozo wa Kongo, baada ya miaka kadhaa ya juhudi ambazo zimeshindwa kuvimaliza vita baina ya Kongo na M23.
Upinzani Kongo wasusia mazungumzo ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa
Huku hayo yakijiri, ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwenyewe, vyama vikubwa vya upinzani vimesusia mazungumzo ya kisiasa yaliyoitishwa na rais wa nchi hiyo Felix Tshisekedi kuanzia jana Jumatatu, kwa lengo la kuunda serikali ya umoja wa kitaifa ili kuyakabili kwa pamoja matatizo yanayoighubika nchi.
Herve Diakiese, msemaji wa chama cha Pamoja kwa ajili ya Jamhuri cha Moise Katumbi, amemtuhumu Tshisekedi kuwa sehemu ya tatizo, na kuongeza kuwa "nyumba inaposhika moto, hujiungi na mchomaji, bali na wazimamoto".
''Iwe mzozo wa makundi yenye silaha, iwe mkwamo wa kisiasa ambavyo vinatusibu leo, sababu zake zinahusiana na kukosa uhalali kwa Rais Tshisekedi, pamoja na taasisi zote za kuteuliwa. Kwa hiyo, Tshisekedi ni sehemu ya tatizo.'' amesema Diakiese.
Vyama vingine vilivyoyasusia mazungumzo hayo ni ECIDE cha Martin Fayulu, na muungano wa FCC unaoongozwa na rais wa Zamani, Joseph Kabila.
Mchambuzi huru wa masuala ya kisiasa Omer Nsongolo, amesema anahofu kuwa hata ikiwa serikali hiyo ya umoja wa kitaifa itafanikiwa kuundwa, kuna hofu bado kuwa Kongo itarudia makosa yake ya zamani, kwani huu sio mchakato wa kwanza wa aina hii kufanyika katika nchi hiyo.