Jopo lachunguza mafungamano ya Emarati na silaha Darfur
29 Aprili 2025Jopo la wataalamu wa Umoja wa Mataifa waliopewa jukumu la kufuatilia vikwazo dhidi ya Sudan linachunguza jinsi vichwa vya vilipuzi na mabomu yaliyosafirishwa kutoka Bulgaria kwenda Umoja wa Falme za Kiarabu yalivyofika katika msafara wa kikosi cha wapiganaji wanamgambo cha Rapid Support Forces RSF.
Hayo ni kwa mujibu wa barua iliyoonekana na shirika la habari la Reuters. Bulgaria imewaambia wataalamu hao kwamba silaha hizo zilizokamatwa katika msafara wa RSF Novemba mwaka uliopita katika eneo la Darfur Kaskazini zilikuwa na nambari ya usajili ya silaha ilizozipeleka katika Umoja wa Falme za Kiarabu 2019.
Bulgaria imesema haikuombwa ruhusa ya silaha hizo kuuzwa na kusafirishwa kwa nchi ama upande wa tatu.
Umoja wa Mataifa umekataa kutoa kauli kuhusu ripoti hiyo. Umoja wa Falme za Kiarabu umekanusha mara kwa mara kwamba unachochea mgogoro kwa kuihami RSF katiak vita vyake dhidi ya jeshi la Sudan.