Jinsi mtiririko haramu wa fedha unavyoathiri ukuaji Afrika
7 Septemba 2025Inakadiriwa kuwa dola bilioni 88 za Marekani, sawa na euro 76 bilioni hutoka Afrika kila mwaka kupitia ukwepaji kodi, utakatishaji fedha na ufisadi, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Mwaka 2015, kiwango hicho kilikuwa dola bilioni 50 (€43 bilioni). Wachambuzi wanasema hali hii inazinyima serikali mapato ambayo yangetumika kuboresha huduma za umma kama afya, elimu na miundombinu.
Viongozi wahamisha fedha kwenye visiwa vya kodi
Christoph Trautvetter, mratibu wa shirika la Kijerumani la Network for Tax Justice, aliiambia DW kuwa Afrika inapoteza mabilioni kwa sababu "makampuni ya kidijitali na wafanyabiashara wa bidhaa ghafi wanahamisha faida zao kwenye mataifa yasio na masharti magumu ya kodi na wakuu wala rushwa wanaficha fedha katika akaunti za siri za nje ya nchi.”
"Hasara ya moja kwa moja ni kubwa zaidi kwa sababu mfumo huu unakuza ufisadi na uhalifu na kudhoofisha nchi ambazo zinapaswa kuhakikisha maendeleo,” alisema Trautvetter, na kuongeza kuwa "wenye nguvu na matajiri Afrika na Kaskazini ya Dunia wananufaika na mfumo huu.”
Alionya pia kuwa "kuna upinzani mkubwa dhidi ya kuhakikisha uwazi na ushirikiano bora au kufanya mageuzi ya kimsingi.”
Ingawa anaamini kuwa hatua zilizochukuliwa bado hazitoshi, Trautvetter alibainisha mafanikio fulani, hasa zaidi ya nchi 100 kukubaliana mwaka 2017 kubadilishana moja kwa moja taarifa za wamiliki wa akaunti za benki.
"Hii inamaanisha sasa benki nyingi kwenye visiwa vya kodi zinapeleka taarifa za wamiliki wa akaunti kwa mamlaka za kodi katika nchi zao,” alisema.
Uwazi zaidi katika udhibiti wa data
Nchi nyingi za Afrika bado zinaanza kutekeleza makubaliano hayo, hivyo data za tathmini bado zinakosekana. "Lakini hii italeta maboresho makubwa katika miaka ijayo,” alisema Trautvetter.
Hatua nyingine chanya ni makubaliano ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa yaliyoanza Agosti 2025, ambayo yanalenga kufafanua masuala kama haki ya kodi ya kimataifa, kodi kwa makampuni makubwa ya kidijitali na ufuatiliaji wa mitiririko ya kifedha haramu.
Licha ya hatua hizi, ripoti ya AU inabainisha kuwa mabadiliko ya siasa za kimaeneo duniani katika kipindi cha miaka 10 iliyopita yameifanya Afrika kuwa dhaifu zaidi.
Vigezo muhimu ni pamoja na mvutano kati ya Marekani na China, janga la COVID-19, vita kati ya Urusi na Ukraine, na athari za siasa za kieneo za mabadiliko ya tabianchi. Aidha, baadhi ya mataifa ya Afrika yanakabiliwa na viwango vikubwa vya madeni ya serikali.
AU imeunda vyombo kadhaa kukabiliana na shughuli hizi haramu. Mbali na jukwaa la ushirikiano wa Afrika, makundi ya kazi yameanzishwa kwa ajili ya kurejesha mali zilizoibwa nje ya nchi na kudhibiti sekta kama madini, ambazo ni hatarishi zaidi kwa uuzaji haramu.
Kwa ngazi ya kitaifa, nchi nyingi za Afrika zimeanzisha vitengo vya uchunguzi wa kifedha au mamlaka maalum za kodi. Lakini matokeo ya AU yanaonyesha taasisi hizi hazijafanya kazi kwa ufanisi kama ilivyotarajiwa.
Mtiririko haramu ukinyonya Afrika
Idriss Linge kutoka Cameroon, afisa wa taasisi ya Tax Justice Network (TJN) yenye makao Uingereza, anakiri kuwa ukwepaji kodi umeiathiri pakubwa Afrika: "Mtiririko haramu wa kifedha upo duniani kote, lakini Afrika imeathirika zaidi kwa sababu bajeti tayari ni finyu,” aliiambia DW.
"Makampuni makubwa yanatumia vibaya sekta za madini, visiwa vya kodi vinawawezesha kulipa kodi kidogo, na ukosefu wa uwazi unaficha yote hayo. Mitiririko haramu ya kifedha ni kama ugonjwa hatari, unanyonya damu ya Afrika,” alisema Linge.
Kwa mujibu wa Linge, nchi zenye rasilimali kama Nigeria, Angola na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ndizo zilizo hatarini zaidi. Nchini Nigeria pekee, mabilioni yamepotea kupitia upotoshaji wa faida katika sekta ya mafuta.
"Fedha hizo zingetosha kutoa maji safi kwa watu 500,000, huduma za usafi kwa 800,000, elimu kwa watoto 150,000 na kuokoa maisha ya zaidi ya watoto 4,000 kupitia huduma bora za afya. Mitiririko haramu ya kifedha si dhana ya mbali — inawanyima watu haki zao,” alisema.
Ingawa AU inakadiria hasara ya kifedha ya Afrika kufikia dola bilioni 88 kila mwaka, Linge anasema hizo huenda ni takwimu za chini mno. "Wakati huohuo, Afrika inalazimika kulipa madeni kwa viwango vya juu vya riba,” alisema, akibainisha kuwa nchi za Afrika hulazimika kukubali riba kubwa zaidi sokoni kuliko uchumi tajiri kwingine.
Kwa kupoteza mapato kupitia ukwepaji kodi na kubanwa na mzigo wa kulipa madeni, nchi nyingi za Afrika hukwama kifedha. Hali hii inazuia juhudi za kulipa mishahara ya walimu na madaktari, kujenga uthabiti wa tabianchi au kufadhili maendeleo.
Kudhibiti mitiririko haramu ya kifedha kutakuwa hatua ya kwanza kuelekea uhuru mkubwa zaidi kwa serikali za Afrika.