Jeshi la Uganda lakanusha tuhuma
20 Septemba 2005Kampala:
Jeshi la Uganda leo limekanusha tuhuma za Shirika la Haki za Binaadamu lenye makao yake makuu mjini New York, Marekani (HRW) kuwa linawatesa raia wanaokabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo. Msemaji wa Jeshi la Uganda, Shaban Bantariza, amesema kuwa Jeshi la Uganda ni safi kwa sababu siku zilizopita Wanajeshi waliokuwa wanavunja haki za Binaadamu wamechukuliwa hatua kali. Bantariza ameongeza kusema kuwa tokea mwaka 2000, Wanajeshi sita wamehukumiwa na Mahakama ya kijeshi baada ya kupatikana na hatia ya vitendo viovu kama vile kuua na kushindwa kuwalinda raia wasiokuwa na makazi ambao ni Wahanga wa vita baina ya Waasi wa Lord’s Resistance Army (LRA) na Wanajeshi wa Uganda. Ripoti ya Shirika la HRW imesema kuwa Wanajeshi wa Uganda hawana nidhamu, wanabaka Wanawake, wanapiga watu, wanawafunga ovyo ovyo na kuwaua raia katika kambi za Wakimbizi huku serikali ya Rais Museveni inaangalia tu na haichukui hatua.