Jeshi la Uganda laingia katika mji mwingine wa Kongo
3 Machi 2025Hatua ya Uganda imejiri chini ya kiwingu cha wasiwasi kwamba vita vya Mashariki mwa Kongo huenda vikatanuka na kuwa vita kamili vya kikanda.
Msemaji wa jeshi la Uganda na masuala ya ulinzi, Felix Kulayigye amewaambia waandishi habari wa shirika la AFP kwamba kikosi cha jeshi kimeingia katika mji wa Mahagi na kinaudhibiti mji huo, ikiwa ni baada ya kupata ombi kutoka jeshi la Kongo. Hii ni kufuatia kuwepo madai kwamba kuna mauaji ya raia yanafanywa na wapiganaji wa kundi la CODECO kwenye eneo hilo.
Hata hivyo, msemaji huyo hakutowa ufafanuzi zaidi kuhusu operesheni ya kikosi cha Uganda. Mahagi ni mji ulioko mkoa wa Ituri unaopakana na Uganda, na ambako kiasi watu 51 waliuwawa Februari 10 na wapiganaji wenye silaha wanaohusishwa na kundi la CODECO, kwa mujibu wa vyanzo vya mashirikia ya kibinadamu na wenyeji.