Jeshi la Sudan lasema limerejesha udhibiti wa mji mkuu
28 Machi 2025Mafanikio hayo yanahitimisha mapigano ya wiki moja ambayo yalishuhudia kuirejesha tena ikulu ya rais, uwanja wa ndege na maeneo mengine ya kimkakati.
Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wa jeshi la Sudan Nabil Abdullah ni kwamba vikosi vya jeshi hilo vimewafurusha wapiganaji wa RSF wanaoongozwa na Mohamed Hamdan Daglo na kuwaondoa katika maeneo ya mji mkuu Khartoum.
Siku ya Jumatano mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan alitangaza kwamba mashambulizi ya hivi karibuni yamefanikiwa kuurejesha mji mkuu baada ya kushindwa kwa majaribio kama hayo mfululizo kwa mwaka mmoja na nusu.
Vita hivyo vya tangu Aprili mwaka 2023 vimesababisha vifo vya maelfu ya watu, na kupelekea zaidi ya milioni 12 kuyahama makazi yao na kusababisha mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu kuwahi kurekodiwa.