Jeshi la Sudan lasema limeinyakua Ikulu mjini Khartoum
21 Machi 2025Katika ujumbe kupitia televisheni ya taifa, msemaji wa jeshi hilo Nabil Abdallah amearifu kuwa vikosi vya nchi hiyo vimewasambaratisha wapiganaji wa upande wa RSF pamoja na zana zao za kivita na kukamata shehena kubwa ya silaha.
Taarifa zinasema kulitokea mapigano makali kati ya pande hizo mbili kabla ya vikosi vya jeshi la Sudan kupata mafanikio, ambayo ndiyo makubwa zaidi tangu kuzuka kwa vita Aprili, 2023.
Soma pia:Hiki ndicho kitasababisha mvutano mpya Sudan Kusini
Picha na video kwenye mitandao ya kijamii ambazo hata hivyo hazijathibitishwa na vyanzo huru vya habari, zimewaonesha wanajeshi wakiwa ndani ya majengo ya ikulu huku wakipongezana.
Eneo la katikati mwa mji mkuu wa Sudan, Khartoum, yaliyo majengo ya ikulu, limekuwa kitovu cha mapigano makali kati ya pande hizo hasimu mnamo miezi ya karibuni.