Jeshi la Sudan lakomboa sehemu kubwa ya Khartoum
9 Februari 2025Jeshi la Sudan limesema, limekomboa sehemu kubwa ya Khartoum Kaskazini huku likiongeza nguvu mapambano yake yanayolenga kuukombowa kikamilifu mji huo mkuu unaoshikiliwa na wanamgambo wa RSF.
Mkuu wa majeshi jenerali Abdel Fattah al-Burhani, Jumamosi alitangaza mipango ya kuunda serikali ya mpito itakayosaidia kutimiza majukumu ya kijeshi na kuwatokomeza kabisa wanamgambo wa RSF nchini Sudan.
Jeshi la Sudan liko vitani na RSF tangu Aprili 2023 na katika wiki za hivi karibuni limefanikiwa kulikomboa eneo kubwa la mji mkuu Khartoum na maeneo yanayozunguuka mji huo yaliyokuwa yameangukia mikononi mwa RSF.
Jenerali Abdel-Fattah al Burhani amesema hatua atakayoichukuwa itafunguwa njia ya kupatikana mageuzi makubwa ya kisiasa yatakayopelekea kufanyika uchaguzi.
Katika mji mkuu, siku ya Jumamosi jeshi lilisema limekomboa wilaya muhimu ya Kafouri iliyoko Kaskazini mwa Khartoum baada ya kuwarudisha nyuma wanamgambo wa RSF kuelekea mji ulioko nje kabisa wa Bahri.
Wilaya ya Kafouri ni moja ya maeneo tajiri kabisa ya Khartoum na imekuwa ngome muhimu kwa RSF na ndiko kunakopatikana mali zinazohusishwa na viongozi wa kundi hilo la wanamgambo,ikiwemo za Abdel Rahim Daglo ambaye ni nduguye Kamanda wa RSF Mohammed Hamdani Daglo.
Rahim Daglo pia ni naibu wa RSF. Katika taarifa ya jeshi la Sudan, msemaji wake Nabil Abdullah alibaini kwamba vikosi vya jeshi na washirika wake Ijumaa walifanikiwa kuwarudisha nyuma wapiganaji wa Daglo kutoka Kafouri na maeneo mengine, kilomita 15 kuelekea mashariki katika eneo la Sharq El Nil.
Mkaazi mmoja karibu na mji huo wa Kafouri alisema, furaha iliyoonekana wakati wanamgambo wa RSF wakiondoka kwenye mji huo ilikuwa haina mfano wake.
Azahir Suleiman mwenye umri wa miaka 43 aliliambia shirika la habari la AFP kwamba wanasubiri huduma zirejee kwenye eneo hilo na majirani zao watakaorejea, lakini pia kuona vita vikimalizika na Sudan kuwa tena na utulivu.Soma pia: Sudan: Je, vita vya umwagaji damu vinaelekea kufikia mwisho?
Mnamo siku ya Alhamisi vyanzo vya jeshi viliiambia AFP kwamba jeshi hilo pia linasonga mbele kuelekea katikati ya Khartoum huku mashahidi wakiripoti kutokea mapambano kwenye eneo hilo na miripuko ilisikika Kusini mwa mji mkuu.
Matukio haya mapya ni moja ya mafanikio makubwa ya jeshi la Sudan tangu vilipozuka vita kati ya mkuu wa majeshi Abdel Fattah al Burhani na aliyekuwa mshirika wake anayeongoza RSF Hamdani Daglo.
RSF iliteka eneo kubwa la Khartoum na maeneo mengine ya kimkakati.
Shirika la kutetea haki za binadamu Ijumaa lilizungumzia wasiwasi wake kuhusu uwezekano wa mapigano ya kulipa kisasi katika maeneo ambayo hivi karibuni yalikombolewa na jeshi, wakati mapigano yakiendelea.
Shirika hilo lilizungumzia wasiwasi wake huo baada ya kupata ripoti juu ya kuwepo orodha inayosabambazwa ya majina ya wanaharakati, watetezi wa haki za binadamu,madaktari na wafanyakazi wa mashirika ya kiutu wanaotuhumiwa kuwa ni washirika wa RSF.
Mgogoro wa Sudan umesababisha uharibifu mkubwa katika taifa hilo,zaidi ya watu milini 12 wameachwa bila makaazi na kuitumbukiza katika mgogoro mkubwa wa kibinadamu ambao haujawahi kutokea, kwa mujibu wa kamati ya Kimataifa ya uokozi.