Jeshi la Kongo, washirika wawadhibiti M23 kuelekea Bukavu
1 Februari 2025Jeshi la Kongo kwa msaada wa jeshi la Burundi lilionekana Ijumaa kudhibiti shinikizo la waasi wanaoungwa mkono na Rwanda wanaotaka kupanua udhibiti wao wa mikoa ya mashariki mwa Kongo katika mashambulizi ya wiki chache yaliyosababisha hofu ya mgogoro mpana wa kikanda.
Mapema wiki hii, waasi wa M23 wanaoongozwa na Watutsi waliiteka Goma, mji mkubwa zaidi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambao ni nyumbani kwa migodi ya dhahabu, coltan, na madini ya shaba. Kisha walielekeza macho yao kwa Bukavu, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kusini, na walipiga hatua kuelekea lengo hilo.
Soma pia:Kongo: Mji wa Bukavu wachukua tahadhari dhidi ya M23
Lakini tangu wakati huo, jeshi la Kongo na washirika wake wamefanikiwa kuwadhibiti waasi hao, vyanzo vitatu, akiwemo Gavana wa Kivu Kusini Jean-Jacques Purusi Sadiki waliliambia shirika la habari la Reuters.
Mmoja wa watu waliokuwa na taarifa za moja kwa moja kuhusu mapigano alisema kikosi cha takribani 1,500 wakiwemo wanajeshi wa Kongo, Burundi, na wapiganaji wanamgambo wa ndani kilitumwa kulinda mji wa Nyabibwe, ulioko kilometa 50 kaskazini mwa Bukavu.
Chanzo hicho kilikataa kutambulika kwa sababu za usalama.
Wakazi wa Bukavu, ambao mara ya mwisho uliangukia kwa waasi mwaka 2004, walisema watu walikuwa wanajitayarisha kwa chakula, tochi, na betri au kukimbilia mpaka wa Burundi.
Raia walioajiriwa na mamlaka kutetea mji huo walikuwa wakifanya mazoezi kuzunguka uwanja wa michezo na kujipanga kwa ajili ya salamu za kijeshi siku ya Ijumaa.
"Tumeumia kwa muda mrefu, tumeumia kwa muda mrefu kwa sababu ya wavamizi ambao ni majirani zetu," alisema mwalimu wa hesabu Habamungu Mushagalusa, mmoja wa kundi la watu takribani 200 walioajiriwa.
"Tuko hapa kulinda ardhi yetu hadi kifo."
Kigali imepinga matokeo ya wachunguzi wa Umoja wa Mataifa kwamba imetuma maelfu ya wanajeshi na vifaa nchini Kongo kuisaidia M23.
Umoja wa Mataifa ulisema Alhamisi kuwa kulikuwa na taarifa za vikosi vya Rwanda kuvuka mpaka na kuelekea Bukavu. Rwanda haikujibu mara moja ombi la kuzungumzia kauli ripoti hizo.
M23 ni kundi la waasi lenye mafunzo bora na silaha za kitaalamu, ndiyo la hivi karibuni katika orodha ndefu ya makundi ya waasi wa Kitutsi yanayoungwa mkono na Rwanda, kutokea katika maeneo tete ya mpaka wa mashariki mwa Kongo kufuatia vita viwili vya mfululizo vilivyotokana na mauaji ya kimbari ya Rwanda ya 1994.
Hofu ya mzozo wa kikanda
Kuongezeka kwa mzozo wa muda mrefu mashariki mwa Kongo kumezua upinzani wa kimataifa dhidi ya Rwanda na msururu wa shughuli za kidiplomasia.
"Hatari ya mgogoro kutanuka katika kanda ni halisi," alisema mwanadiplomasia mmoja wa Kiafrika Ijumaa. "Majeshi ya Rwanda, Kongo, na Burundi tayari yanapigana katika ardhi ya mashariki mwa Kongo."
Ufaransa ilitarajiwa kuwasilisha rasimu ya azimio katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Ijumaa ili kuishinikiza Rwanda kuondoa vikosi vyake, alisema Balozi wa Ufaransa kwa Umoja wa Mataifa, Nicolas de Riviere.
Wakati wa mkutano wa kilele Ijumaa, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) yenye wanachama 16 ilionyesha wasiwasi na kuomba kufanya mkutano wa pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu suala hilo.
SADC pia ilijadili hasara kubwa kwa vikosi vyake vya pamoja vinavyohudumu katika kanda hiyo ambavyo vilipewa jukumu la kuzuia waasi wa mashariki mwa Kongo. Jumuiya hiyo imeomba mawaziri wa ulinzi wa nchi zinazochangia wanajeshi waende Kongo kuhakikisha usalama wa vikosi na kurejeshwa kwa majeruhi.
Umoja wa Mataifa ulisema Ijumaa kuwa mgogoro huu umeongeza ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwemo mashambulizi ya dhidi ya watu waliokimbilia kwenye kambi za wakimbizi, mauaji ya kikatili na ripoti za ubakaji wa kikatili na vitendo vingine vya unyanyasaji wa kingono na wanajeshi wa Kongo.
Soma pia: Kiongozi wa DRC asema jeshi lake linapambana vikali dhidi ya mashambulizi ya M23
Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Umoja wa Mataifa, Jean-Pierre Lacroix, alisema kwa ujumla amani, maji na umeme vimerudi katika mji wa Goma ingawa mji bado ni "tete na yenye kubadilika kila wakati."
Uwanja wa ndege haukuwa ukifanya kazi kwa sababu ya uharibifu, na walinda amani wa Umoja wa Mataifa walikuwa wakihifadhi raia wengi katika vituo vyao, aliongeza.
Burundi, Uganda pia zavutwa kwenye mzozo
Vikosi vya Burundi vinaviimarisha vikosi vya Kongo, hasa katika mkoa wa Kivu Kusini, kwa ombi la serikali ya Kinshasa. Rwanda imekadiria idadi yao kuwa 10,000, vyanzo vya Umoja wa Mataifa vinakadiria kuwa ni maelfu kadhaa na afisa wa Burundi, ambaye alitaka kutotajwa, alisema walikuwa 8,000 hadi 10,000.
Umoja wa Mataifa umesema mapigano kati ya majeshi ya Rwanda na Burundi nchini Kongo yanatishia hatari ya vita vya kikanda kama vile vilivyoua mamilioni kati ya 1996 na 2003, wengi wao kutokana na njaa na magonjwa.
Jeshi la Burundi limekataa kutoa tamko kuhusu matukio ya wiki hii nchini Kongo.
Uganda, ambayo pia ina vikosi mashariki mwa Kongo kwa ajili ya kushughulikia waasi wa Uganda walioko huko, ilisema Ijumaa itatumia "mkakati wa kujilinda" kutokana na mapigano kati ya jeshi la Kongo na M23.
Mataifa makuu ya dunia ikiwemo Marekani, Uingereza, na Ufaransa yametoa wito wa kumaliza mapigano nchini Kongo na yamejaribu kumshinikiza Rais wa Rwanda Paul Kagame kusitisha msaada wake kwa M23.
Baada ya mkutano na Rais wa Kongo Felix Tshisekedi mjini Kinshasa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Noel Barrot alikutana na Kagame Ijumaa. Baadaye ofisi ya Rais wa Rwanda ilisema walijadili "njia za kukuza amani katika kanda" bila kutoa maelezo zaidi.
Wachambuzi wanasema kuwa kukataa kwa mataifa makubwa kuchukua hatua dhidi ya Rwanda, changamoto za kimataifa, na hali halisi ya kijeshi ndani ya Kongo kutasababisha changamoto katika juhudi za kuwashinda waasi.
Chanzo: rtre,apa,dpa,afpe