Jeshi la kimapinduzi Iran laapa kulipiza kisasi
23 Septemba 2018Iran imewahoji wanadiplomasia kutoka nchi tatu za Umoja wa Ulaya Jumamosi usiku kufuatia shambulio lililosababisha vifo lililolengwa dhidi ya gwaride la kijeshi. Iran inazilaumu nchi za kigeni kuhusika na shambulio hilo. Mabalozi wa Denmark,Uholanzi na Uingereza walihojiwa kwa mujibu wa shirika la habari la Iran IRNA ambalo limetowa taarifa hilo leo Jumapili.
Kundi la wanamgambo la al-Ahvazieh limedai kuhusika na shambulio hilo ambalo lilisababisha watu wapatao 25 kupoteza maisha na wengine 60 wakajeruhiwa wakiwemo watoto. Uongozi nchini Iran unadai kwamba Denmark, Uholanzi na Uingereza zimekuwa zikiwahifadhi wanachama wa kundi hilo la wanamgambo. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Bahram Ghassemi amenukuliwa akisema kwamba hatua ya Umoja wa Ulaya ya kutoweza kuliorodhesha kundi hilo la wanamgambo katika orodha ya makundi ya kigaidi kutokana na kwamba halijawahi kufanya uhalifu katika nchi za Ulaya ni kitu kisichokubalika.
Msemaji huyo wa mambo ya nje wa Iran amehoji kwa nini mashambulizi yanapotokea Ulaya yanapewa uzito mkubwa na kuangaziwa zaidi lakini ni tafauti mashambulizi yanapotokea kwengine. Balozi wa Denmark nchini Iran Danny Annan amethibitisha kushiriki mkutano ulioitishwa katika wizara ya mambo ya nje mjini Tehran Jumamosi usiku ingawa hakuna maelezo mengi zaidi yaliyotolewa.
Kiongozi wa juu kabisa nchini Iran Ayatollah Ali Khamenei juu ya shambulio hilo la Ahvaz, amelaumu kile alichokiita njama ya tawala zinazoungwa mkono na Marekani katika kanda hiyo ambazo zinataka kuchochea ukosefu wa Usalama ndani ya Iran. Jeshi la ulinzi la kimapinduzi ni kikosi maalum kinachoongozwa na Khamenei binafsi na ambacho kinajiangalia kama ndicho kinachobeba dhamana ya kuilinda Jamhuri ya kiislamu ya Iran. Jeshi hilo limeahidi kulipiza kisasi.
Gwaride la Jumamosi lilofanywa na wanajeshi hao lililoshambuliwa lilifanyika kuadhimisha mwanzo mwa vita vya Iran na Iraq vilivyotokea 1980, tukio la maadhimisho ambalo lilifanywa pia katika maeneo mengine ya Iran. Rais Hassan Rouhani kwa upande mwingine alitoa tamko Jumapili na kusema kwamba nchi kadhaa ambazo ni washirika wa Marekani katika Ghuba hiyo ya uajemi ndio walioko nyuma ya shambulio hilo. Inatajwa kwamba huenda Rouhani amezilenga Saudi Arabia, Umoja wa falme za kiarabu au Bahrain kutokana na kuwa ndizo nchi washirika wa karibu wa kijeshi wa Marekani wanaoitazama Iran kama adui wa kanda hiyo ya Ghuba kutokana na hatua yake ya kuunga mkono makundi ya wanamgambo katika eneo zima la Mashariki ya kati.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri: John Juma