Israel: Shambulizi la hospitali liliilenga kamera ya Hamas
27 Agosti 2025Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi, askari waliamua kuchukua hatua dhidi ya kamera hiyo, na kuongeza kuwa wakati sita kati ya waliouawa walikuwa "magaidi," jeshi "linajutia" madhara yoyote yaliyosababishwa kwa raia. Madai ya Israel hayawezi kuthibitishwa kwa njia huru, na kuzishambulia hospitali ni uhalifu chini ya sheria za kimataifa.
Shambulizi hilo lililofanywa mara mbili – ambapo waandishi habari watano na wafanyakazi wa misaada ni miongoni mwa watu 20 waliouawa – limelaaniwa na jumuiya ya kimataifa, wakiwemo baadhi ya washirika wa karibu wa Israel.
Mashirika ya haki za binadamu yameishutumu Israel kwa kueneza taarifa potofu ili kuhalalisha mauaji ya raia, waandishi wa habari na wafanyakazi wa misaada huko Gaza.
Maandamano yashuhudiwa Israel
Maelfu ya waandamanaji walikusanyika mjini Tel Aviv, kuishinikiza serikali kukomesha vita huko Gaza na kufikia makubaliano ya kuwarejesha nyumbani mateka, wakati baraza la mawaziri la usalama lilipokutana.
Kufuatia mkutano huo wa baraza la mawaziri Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu baadaye alizungumza kwenye tukio moja jana jioni, lakini hakuwa muwazi kuhusu nia ya serikali. "Tumekuwa kwenye kikao cha baraza la mawaziri na sifikirii kama naweza kufafanua sana lakini nitasema jambo moja: Ilianzia Gaza, na itaishia Gaza. Hatutawaacha hao magaidi huko. Tutawaokoa mateka wao wote. Watahakikisha kwamba Gaza haitakuwa tishio tena kwa Israel." Amesema Netanyahu. Vyombo vya Habari vya Israel vilisema mkutano huo haukutoa maamuzi ya wazi.
Israel inakabiliwa na shinikizo kimataifa kuhitimisha operesheni zake za kijeshi Gaza.
Mjumbe maalum wa Donald Trump Steve Witkoff amesema rais huyo wa Marekani ataandaa leo Jumatano mkutano wa kujadili mipango ya baada ya vita katika Ukanda wa Gaza ulioharibiwa vibaya.
Witkoff amesema ipo haja ya kuwepo na makubaliano wakati vita kati ya Israel na Hamas vikiendelea. "Kumekuwa na mpango mezani kwa wiki sita au saba zilizopita ambao ungewaachilia mateka 10 kati ya 20 ambao inadhaniwa wako hai. Na ni Hamas ambao walichelewesha mchakato huo, na ni Hamas ambao sasa wanasema wanakubali mpango huo. Na nadhani, kwa kiasi kikubwa, wanasema hivyo na kubadili mawazo yao, kwa sababu Israel inawawekea shinikizo kubwa." Amesema Witkoff.
Mapema mwezi huu, Baraza la mawaziri la usalama liliidhinisha mpango wa kutanua operesheni za kijeshi na hatimaye kuchukua udhibiti wa mji wa Gaza, hatua iliyozusha hofu kuhusu usalama wa mateka na hivyo kuzuka wimbi jipya la maandamano ambayo yameshuhudia maelfu ya watu wakiingia mitaani huko Israel. Mpango huo umekosolewa pia vikali na jumuiya ya kimataifa.
Wanadiplomasia wa zamani watoa wito dhidi ya Israel
Barua ya wazi iliyosainiwa na mabalozi na wafanyakazi 209 wa zamani wa Umoja wa Ulaya na nchi wanachama imetoa wito wa kutekelezwa mara moja kwa hatua za Umoja wa Ulaya dhidi ya Israel kuhusu kile wanachosema ni vitendo vyake haramu huko Gaza na Ukingo wa Magharibi.
Barua hiyo imetoa wito wa kutekeleza kwa hatua tisa zilizopendekezwa na Umoja wa Ulaya dhidi ya serikali ya Israel.
Miongoni mwa mapendekezo haya ni kusimamishwa au kufutiliwa mbali kwa leseni ya kuuza silaha kwa Israel na kusitishwa kwa ufadhili wa miradi ya kitaifa inayohusisha mashirika ya Israel.
Barua hiyo ilitaka kutekelezwa kwa vikwazo kwa misingi ya haki za binadamu na sheria za kukabiliana na ugaidi ambazo zitajumuisha marufuku ya viza na kufungia mali.
Barua hiyo iliyotumwa kwa viongozi wa nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya na ngazi za uongozi wa Halmashauri Kuu ya Ulaya, miongoni mwa nyinginezo, ilifuatia barua nyingine ya wazi iliyotumwa mwishoni mwa Julai.
AP, AFP, Reuters, DPA