Jeshi la Israel laendelea kuishambulia Gaza
5 Septemba 2025Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, amesema mashambulizi dhidi ya jengo hilo ni onyo la mwanzo na kwamba operesheni hiyo ya kijeshi itakapoimarishwa, itakuwa vigumu kuisimamisha.
Matamshi yake yanakuja siku chache baada ya Israeli kuanza kuhamasisha maelfu ya askari wa akiba na kurudia onyo lake la uhamaji kama sehemu ya mpango wake wa kupanua mashambulizi katika Jiji la Gaza na ngome nyingine za Hamas, hatua ambayo imeibua upinzani mkali wa ndani ya nchi na shutuma za kimataifa.
Israel yasema imeshambulia jengo linalotumika kwa shughuli za Hamas
Palestina imethibitisha kuwa shambulizi hilo la leo la Israel, lililenga jengo la Mushtaha jijini Gaza, lililoko katika eneo la kusini mwa viunga vya Rimal.
Jengo hilo tayari lilikuwa limekabiliwa na mashambulizi ya Israel na picha za kabla ya shambulizi hilo zilionyesha paa lake likiwa limeharibiwa kabisa.
Israel imesema ilishambulia jengo hilo kwa sababu lilitumika na Hamas kwa shughuli zake za ufuatiliaji.
Hamas yato video za mateka wawili
Kundi la Hamas, leo limetoa video inayowaonesha mateka wawili wa Kiisraeli huko mjini Gaza. Video hiyo imemuonyesha mateka mmoja, Gilboa-Dalal, akiwa kwenye gari, na wakati mmoja akiungana na mateka mwingine, Alon Ohel.
Gilboa-Dalal anasikika kwenye video hiyo akiomba vita viishe na wao kurejea kwa familia zao.
Gilboa-Dalal alionekana mara ya mwisho katika video zaidi ya miezi sita iliyopita akiwa pamoja na mateka mwingine Evyatar David, walipokuwa wakitazama mateka wengine wakiachiliwa huru wakati wa kipindi cha kusitisha mapigano.
Huku wasiwasi juu ya mateka ukiendelea, Israel imeendeleza mashambulizi yake kote katika Ukanda wa Gaza.
Marekani yawekea vikwazo mashirika matatu ya Palestina
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, jana aliyaweka mashirika ya Kipalestina ya Al-Haq, Kituo cha Haki za Binadamu cha Al Mezan, na Kituo cha Haki za Kibinadamu cha Palestina chini ya agizo rasmi la rais linalolenga kuziwekea vikwazo taasisi zinazosaidia uchunguzi wa ICC dhidi ya viongozi na raia wa Israel.
Rubio amesema kuwa mashirika hayo yamehusika moja kwa moja na juhudi za Mahakama hiyo ya ICC za kuchunguza, kutaka kuwakamata, kuwaweka kizuizini au kuwafungulia mashtaka raia na viongozi wa Israel, bila ridhaa ya Israel.
ICC tayari imeomba vibali vya kukamatwa kwa viongozi wa Israel
Hatua hiyo ni ya hivi karibuni zaidi ya juhudi za Marekani kuitingisha Mahakama ya ICC, ambayo imeomba vibali vya kukamatwa kwa maafisa wa ngazi za juu wa Israel, akiwamo Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na waziri wa zamani wa ulinzi Yash Golav, kutokana na tuhuma za uhalifu wa kivita huko Gaza. Mahakama hiyo pia iliomba kukamatwa kwa viongozi wa Hamas, lakini sasa wote wameshauawa na jeshi la Israel.