Jeshi la Israel kusalia katika Ukingo wa Magharibi
23 Februari 2025Israel imesema wanajeshi wake watasalia katika kambi za wakimbizi za Ukingo wa Magharibi kwa mwaka ujao, na kutangaza upanuzi wa operesheni za kijeshi ikiwa ni pamoja na kupeleka vifaru, baada ya maelfu ya Wapalestina kuyahama makazi yao.
Mwezi mmoja uliopita wanajeshi wa Israel walianza uvamizi mkubwa dhidi ya wanamgambo wa Kipalestina katika Ukingo wa Magharibi, baada ya kuanza kwa makubaliano ya kusitisha vita katika Ukanda wa Gaza, eneo jingine la Wapalestina.
Operesheni ya Israel katika Ukingo wa Magharibi inahusisha kambi nyingi za wakimbizi karibu na miji ya Jenin, Tulkarem na Tubas. Kulingana na Waziri wa ulinzi wa Israel, Israel Katz, Wapalestina alfu 40,000 wameondoka katika makambi ya wakimbizi katika Ukingo wa Magharibi ambayo sasa yamebaki matupu.
Katz ametoa amri ya kusalia kwa wanajeshi wa Israel ili kuzuia kurejea kwa wakaazi na kuzuka upya kwa ugaidi.