India yaionya Pakistan juu ya kukiuka makubaliano
12 Mei 2025Onyo hilo limetolewa na afisa mwandamizi wa jeshi la India, na kwa upande mwengine msemaji wa jeshi la Pakistan amekanusha kuwepo kwa ukiukaji wowote wa kusitisha mapigano.
Mkurugenzi wa operesheni za kijeshi wa India ametoa onyo hilo wakati usitishati wa mapigano kwa saa 24 ukitekelezwa baada ya pande zote mbili kulaumiana kwa ukiukaji wa awali wa makubaliano hayo usiku wa kuamkia Jumamosi.
Soma pia: India na Pakistan zaendelea kushambuliana
Makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyotangazwa Jumamosi yalifuatia siku nne za mapigano makali kati ya majirani hao wanaomiliki silaha za nyuklia. Katika mapigano mabaya zaidi kuwahi kutokea kwa takriban miongo mitatu, India na Pakistan zilishambuliana kwa makombora na droni na kulenga vituo vya kijeshi vya kila upande, na kusababisha vifo vya karibu watu 70.
Diplomasia na shinikizo kutoka Marekani imesaidia kufanikisha makubaliano ya kusitisha mapigano katika wakati ambapo ililionekana nchi hizo mbili zitatumbukia kwenye mzozo mbaya zaidi.