JERUSALEM:Wapinzani wa Israel kuondoka Gaza kukaidi amri ya kuzuia maandamano.
2 Agosti 2005Huko nchini Israel watu wanaopinga mpango wa nchi hiyo kujiondoa kutoka eneo la Ukanda wa Gaza,wamesema watakaidi amri inayowakataza kutoandamana leo katika baadhi ya makazi ya walowezi wa Kiyahudi katika mji wa Gaza.
Viongozi walioandaa maandamano hayo wamesema watakachofanya ni kujaribu kuelekea katika eneo kuu la makazi ya walowezi la Gush Katif.Zaidi ya polisi elfu 15 wakishirikiana na wanajeshi wamewekwa katika eneo la Ukanda wa Gaza kuwazuia watu wanaotaka kuuhujumu mpango huo wa Israel wa kuondoka katika maeneo hayo.
Kucha jana polisi wamekuwa katika mazungumzo ya kuwashawishi wapinzani hao na kufanikiwa kuwaruhusu kufanya maandamano ya kidemokrasia leo jioni katika mji wa Sderot kusini mwa Israel na baadae kutakiwa kutawanyika haraka baada ya maandamano hayo.
Mpango wa Israel kuondoka katika maeneo ya Gaza umepangwa kuanza wiki mbili zijazo.Serikali ya nchi hiyo imejaribu kuzuia mapingamizi mengi kutoka kwa watu wanaopinga mpango huo,kwa vile imesema kuruhusu upinzani huo kunaweza kuchochea ghasia zaidi kutoka kwa Wapalestina.