Jerusalem: Watu wanne wafa katika mashambulizi ya risasi
8 Septemba 2025Wahudumu wa afya wamethibitisha juu a kuuawa watu hao wanne katika mashambulizi ya risasi mjini Jerusalem baada ya washambuliaji kufyatua risasi ndani ya basi katika eneo la makutano kaskazini mwa mji wa Jerusalem ambalo kwa kawaida huwa lina shughuli nyingi.
Wahudumu wa afya pia wamefahamisha kuwa watu sita kati ya jumla ya watu15 walijeoruhiwa wako katika hali mahututi. Polisi wamesema washambuliaji wawili walilengwa na kuuawa mara tu baada ya mashambulizi yalipoanza.
Wakati huohuo Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz kwa mara nyingine ametoa onyo kali kwa wanamgambo wa kundi la Hamas kwamba siku ya Jumatatu watashuhudia kimbunga cha mashambulizi katika mji wa Gaza City, ambako jeshi la Israel linatarajiwa kuyadodonsha maghorofa zaidi katika mji huo.
Katz, amejigamba kwa kusema maghorofa katika Gaza City yatatetemeka. Amewataka Hamas wawaachilie mateka na waweke chini silaha zao au sivyo Gaza itaangamizwa.
Naye Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sanchez, siku ya Jumatatu ametangaza hatua tisa zinazolenga kukomesha "mauaji ya halaiki huko Gaza", ikiwa ni pamoja na vikwazo vya silaha kwa Israel na kuzipiga marufuku kutumia bandari za Uhispania, meli zinazobeba mafuta kwa ajili jeshi la Israel.
Sanchez katika hotuba yake kwa njia ya televisheni amesema hatua hizo zitawezesha kukomesha mauaji ya kimbari huko Gaza, kuwawajibisha wahusika wa maafa katika eneo hilo na kuonyesha uungaji mkono kwa watu wa Palestina.
Kwa upande wake Rais wa Marekani Donald Trump amewaambia wapiganaji wa kundi la Hamas kwamba ametoa onyo la mwisho hapo siku ya Jumapili kuwa lazima wakubali makubaliano ya kuwaachilia mateka huko Gaza.
Katika taarifa iliyotolewa muda mfupi baadaye, Hamas ilijibu kwa kusema iko tayari kukaa kwenye meza ya mazungumzo kwa kuzingatia baadhi ya mawazo ya upande wa Marekani yanayolenga kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano.
Vyanzo: AP/DPA/AFP