JERUSALEM: Wanajeshi na polisi wapelekwa Gaza kulinda usalama
1 Agosti 2005Wanajeshi na polisi nchini Isreal wameanza kupelekwa katika eneo la mkanda wa Gaza kuzuia maandamano ya kupinga mpango wa kuyaondoa makazi ya walowezi wa kiyahudi kutoka Gaza. Duru za usalama nchini humo zinasema wanajeshi elfu 17 na polisi elfu 8 watashiriki katika oparesheni hiyo kusini mwa Israel itakayoanza hapo kesho, siku 15 kabla mpango wa kuyaondoa makazi ya wayahudi kuanza huko Gaza.
Kundi la Yesha linaloandaa maandamano hayo limesema yataanza katika mji wa kusini wa Sderot na waandamanaji watatembea hadi makazi ya Gush Katif kusini mwa Gaza. Maandamano hayo ni juhudi za mwisho za kumshinikiza waziri mkuu wa Israel, Ariel Sharon, kubadili msimamo wake juu ya mpango wa kuyaondoa makazi ya wayahudi kutoka ardhi ya wapalestina, ikiwa ni mara ya kwanza tangu Israel ilipoanza kuyakalia maeneo ya Gaza na ukingo wa magharibi mnamo mwaka wa 1967.