Jerusalem. Waandamanaji waapa kuendelea na maandamano yao hadi Gaza.
20 Julai 2005Maelfu ya waandamanaji wakipinga dhidi ya mpango wa Israel wa kujiondoa kutoka eneo la ukanda wa Gaza wameahidi kuendelea na maandamano yao hadi katika makaazi ya walowezi yaliyoko Gaza , licha ya serikali kuyapiga marufuku.
Kiongozi wa walowezi wa Kiyahudi amewaambia waandishi wa habari kuwa wako tayari kuendelea na upinzani wao na kupambana na majeshi ya usalama kwa muda wote hadi wakubaliwe kufanya maandamano yao hadi Gaza.
Majeshi ya Usalama yamewazunguka waandamanaji hao umbali wa kilometa 15 mashariki ya Gaza, ili kuwazuwia kuendelea na maandamano yao ndani ya eneo hilo.
Yameripotiwa kutokea mapambano kiasi kati ya polisi wa Israel na waandamanaji.
Watu walioshuhudia wamesema kiasi cha watu 16 wenye msimamo mkali wa kizalendo wamekamatwa.