JERUSALEM: Uturuki na Israel kurudisha urafiki.
2 Mei 2005Waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan katika ziara yake ya kwanza ya kiserikali nchini Israel, amefanya mazungumzo na mwenyeji wake waziri mkuu wa Israel Ariel Sharon.
Viongozi hao wawili wamekubaliana kuzidisha ushirikiano baina ya nchi zao katika ziara ambayo inachukuliwa kama hatua ya kurudisha uhusiano ambao ulizorota tangu mwaka jana wakati ambapo waziri mkuu wa Uturuki alipo ishutumu Israel hadharani kuwa inahusika na vitendo vya kigaidi.
Kiongozi huyo wa Uturuki baadae alitoa ahadi ya kuisaidia Palestina katika shughuli za ujenzi katika ukanda wa Gaza mara tu Israel itakapo kamilisha mpango wake wa kuwahamisha masetla wa kiyahudi baadae mwaka huu.
Mapema Erdogan alitoa heshima zake kwa wahanga waliouwawa na mafashisti wa Nazi katika makaburi ya kihistoria ya Yad Vashem.