Jenerali Muhoozi athibitisha kumshikilia mlinzi wa Bobi Wine
2 Mei 2025Kauli za mkuu wa majeshi ya Uganda Jenerali Muhoozi Kainerugaba kupitia mtandao wa X kuhusu kumshikilia Eddie Mutwe mlinzi mkuu wa kiongozi wa upinzani Bobi Wine katika chumba cha siri na kumlazimisha asujudu mbele ya picha ya Rais Museveni kabla ya kupewa chakula, kumfundisha lugha ya Kinyankole, na hata kutishia kumkebei, zimeibua mseto wa hasira, hofu na fedheha miongoni mwa Waganda, zikielezwa kama ishara ya kuongezeka kwa ukatili dhidi ya wapinzani wa serikali.
Tangu kutekwa kwa Edward Sebuwufu mwishoni mwa wiki iliyopita, vyombo vya usalama vikiongozwa na polisi vimekanusha kufahamu kule aliko. Mlinzi huyo mkuu wa kiongoz wa chama kikuu cha upinzani Robert Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine alitekwa na watu wasiojulikana siku sita zilizopita alipokuwa akienda kujumuika na watu wa familia yake.
Soma zaidi: Vuguvugu la MK la Uganda lajigeuza asasi ya kiraia
Mara tu baada ya kisa hicho Bobi Wine alitoa taarifa kwa umma. Ila msemaji wa polisi Kituma Rusoke aliwaambia wanahabari kwamba polisi haikuwa na habari rasmi kuhusu kule aliko bwana huyo.
Kituma Rusoke ''hata mimi nimesikia tu kwamba Eddie Mutwe alitekwa na hatujui aliko tukipata habari tutawafahamisha''
Usiku wa mkesha wa leo Ijumaa mwanawe rais Museveni ambaye pia ni mkuu wa majeshi Jenerali Muhoozi Kainerugaba alisambaza ujumbe kwenye ukurasa wake wa X akimjibu Bobi Wine kwamba yeye ndiye anamshikilia mlinzi wake mkuu katika handaki ya jumba fulani.
Soma zaidi:Uganda: Vikosi vya usalama vyawakabili wanahabari
Ili kuthibitisha hilo ameambatanisha picha ya Eddie Mutwe kinyume na mwonekano wake unaofahamika na umma wa masharubu amenyolewa upara na uso wake kuonyesha hali ya mwanamume anayepitia katika machungu mengi katika kizuizi alimo.
Kitendo hicho kimewaghadhabisha wengi
Mwanzoni watu wengi walidhani picha hiyo ni mzaha lakini kufuatia ujumbe zaidi wa Jenerali huyo sasa wamethibitisha ni kweli. Picha hiyo imewatoa machozi watu mbalimbali huku wakielezea hisia mseto walizo nazo za huruma, hofu na hasira.
Kile ambacho pia kimeibua ghadhabu hasa miongoni mwa watu wa kabila la Ankole ni majigambo ya jenerali huyo kwamba kwa sasa Eddie Mutwe anafunzwa lugha ya Kinyankole na kulazimishwa kupigia picha ya rais Museveni saluti kabla ya kupewa chakula.
Soma zaidi:Kampala: Makao Makuu ya chama cha Upinzani yavamiwa
Kupitia kwenye mitandao ya kijamii, watu kadhaa wa jamii hiyo wameshutumu vikali hatua hiyo wakisema inawatia katika hali ya uhasama na watu wa jamii zingine. Wamejitenga kabisa na msimamo wake.
Gorreth Namugaa Mbunge wa chama cha NUP amewataka raia wote wa Uganda kuungana kupinga vitendo vya mkuu wa majeshi ambavyo anaelezea vinadhihirisha kwamba viongozi hawaheshimu tena katiba na sheria za nchi.
Gorreth Namugaa ''Manyanyaso dhidi ya Eddie yanatupa changamoto sisi sote wananchi. Viongozi mko wapi kutetea katiba ya nchi kulingana na vitendo hivi''
Hadi wakati wa kuandaa taarifa hii, Bobi na chama chake hawakuwa wametoa tamko rasmi ila tu kauli aliyotoa kumjibu na Jenerali Muhoozi kwenye ukurasa wa X kwamba ‘Time will tell’ yaani wakati utaamua. Lubega Emmanuel DW Kampala.