Je utawala wa Trump unaandika upya historia Marekani?
1 Septemba 2025Wachambuzi wanakosoa kuwa matamshi ya kiongozi huyo yanabainisha kosa jingine la kihistoria ndani ya utawala wa Trump.
Katika mtandao wa X akaunti iitwayo "Republicans against Trump” iliandika Vita vya Pili vya Dunia vilitamatika kwa Ujerumani na mshirika wake Japan kusalimu amri bila masharti na si kwa majadiliano" ujumbe huu ukisindikizwa na kipande cha video kikionesha mahojiano ya makamu wa Rais Vance.
Mnamo Mei 8, 1945, Ujerumani ya Kinazi ilisalim amri bila masharti baada ya dikteta Adolf Hitler kujiua. Mshirika wake Japani alisalimu amri baadaye mwezi Agosti, baada ya Marekani kulipua mabomu ya nyuklia Hiroshima na Nagasaki. Maoni hayo ya kiongozi huyo wa juu Marekani yanatajwa kubainisha kosa jingine la kihistoria ndani ya utawala wa Trump.
Wachambuzi wanasema Rais Trump mara kadhaa amekuwa akipotosha historia ili kuendana na maoni yake na ameshindwa kwa mara kadhaa kushinikiza taasisi kama vile makumbusho zikiakisi mitazamo yake huku akizikosoa kuonesha historia ya Marekani-- hasa masuala ya utumwa katika mtazamo hasi.
Kikosi cha kuhakiki ukweli cha DW kimechunguza baadhi ya madai ya kihistoria ambayo yamejaa utata kutoka kwa Rais Trump. Tuanze na madai ya mjomba wake na "Unabomber”. Ted Kaczynski, mmoja wa magaidi wa ndani waliotajwa zaidi kwa jina la "Unabomber,” aliua watu watatu na kuwajeruhi wengine 23 kwa kutuma mabomu kupitia barua, akiwalenga hasa wanasayansi. Alikiri kutuma mabomu 16 katika kipindi cha karibu miongo miwili.
Matamshi ya Trump hasa kuhusu vita vya Iraq yameendelea kukosolewa
Mnamo Julai, Trump alidai katika mkutano Pittsburgh, Pennsylvania kuwa mjomba wake marehemu John, aliyewahi kuwa profesa katika MIT, alimfundisha Kaczynski. Lakini ukweli ni kwamba Kaczynski alisoma Harvard kisha Chuo Kikuu cha Michigan. Mjomba wa Trump alifariki mwaka 1985, ilhali Kaczynski alikamatwa mwaka 1996. Historia hiyo imekanushwa na vyombo kadhaa vya habari.
Vipi kuhusu madai ya kupotosha juu ushuru na mdodoro mkubwa wa kiuchumi nuduniani napo kuna ulakini kwenye madai ya Trump. Katika kikao cha baraza la mawaziri Julai, Trump alisema Mdororo Mkuu usingetokea iwapo Marekani ingelinda ushuru wa forodha, na kudai kimakosa kwamba ushuru wa forodha ulirejeshwa "baada ya Mdororo.”
Lakini ukweli ni kwamba Mdororo Mkuu ulianza mwaka 1929 na kudumu karibu muongo mzima. Sheria ya Smoot-Hawley ya mwaka 1930, iliyolenga kulinda biashara za Marekani, ilipandisha ushuru wa forodha na kusababisha zaidi ya nchi 20 kulipiza kwa ushuru wao jambo lililoimarisha zaidi mgogoro wa kiuchumi wa dunia. Kabla yake, tayari kulikuwa na Sheria ya ushuru ya mwaka 1922 iliyoweka ushuru mkubwa wa bidhaa zinazoingizwa.
Katika uga wa kimataifa nako kuna mgagaiko katika matamshi ya rais Trump hasa kuhusiana na vita vya Iraq ameendelea kukosolewa kwa madai yake kuhusu historia. Amedai mara kwa mara kwamba alipinga uvamizi wa Iraq mwaka 2003, na mnamo mwezi Juni alirejea kauli hiyo akisema: "Nilipinga sana Iraq. Nilisema kwa uwazi: ‘Msivamie, msivamie, msivamie.'” Hata hivyo ripoti za CNN, Buzzfeed na Washington Post zinaonyesha awali aliunga mkono hatua hiyo kabla ya kubadili msimamo.
Wakati huo huo, Trump amesaini agizo la kuchunguza makumbusho ya Smithsonian, akitaka yaondoe kile anachokiita "itikadi zisizo za kizalendo.” Hatua hiyo imeibua upinzani kutoka mashirika zaidi ya 150 ya kitamaduni na mamia ya watu binafsi waliotetea uhuru wa kisanii na kuonya dhidi ya shinikizo la kisiasa.